Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amewataka wachezaji wake kutoridhika na ushindi wanaoupata kwenye mechi za Ligi Kuu NBC, badala yake waongeze bidii ili kuhakikisha wanajiweka katika mazingira mazuri ya kutetea taji hilo.
Yanga ndio vinara wa ligi hiyo kwa sasa wakiwa na pointi 53 katika michezo 20 waliyocheza hadi sasa, ikiwa imesalia michezo 10 kabla ya ligi kumalizika.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo kocha huyo raia wa Tunisia ameeleza kuwa kadri siku zinavyokwenda ushindani umeongezeka na timu nyingi zimekuwa zikiwapania hivyo ni lazima kuongeza umakini ili kuhakikisha hawapotezi mchezo.
“Unajua ligi inaelekea mwisho, timu nyingi zinataka kumaliza kwenye malengo yao ndio maana nawataka wachezaji wangu kutobweteka hasa katika kipindi hiki ambacho ligi inaelekea ukingoni na ushindani umekuwa mkubwa mno,” alisema Nabi.
Kocha huyo ameeleza kuwa kwa namna presha ilivyo kwa sasa angependa kuona kila mchezaji wake anajitoa kwa asilimia 100, ili kupata pointi tatu na siyo sare au kupoteza mchezo sababu itawapa nguvu wapinzani wao Simba kutokana na pengo la pointi kupungua.
Pia Nabi amezungumzia mchango wa wachezaji waliosajiliwa dirisha dogo lililofungwa siku mbili zilizopita ambapo ameeleza kuwa umeongeza kitu kwenye timu yake na hiyo imemwongezea machaguo hasa katika eneo la kiungo.
“Kila mchezaji tuliyemuongeza kwenye dirisha dogo hakuja kwa bahati mbaya, kuna kitu tumeamini atakuja kutuongezea kufikia malengo yetu na tayari tumemuona Mudathir Yahya na Kennedy Musonda hivi karibuni pia tutamshuhudia Mamadou Doumbia na Metacha Mnata hawa wote hawakuja kwa bahati mbaya, kuna kitu ambacho wanakuja kukiongeza kwetu na ni usajili muhimu,” alisema Nabi.
Kutokana na ushindani wa kuwania ubingwa ulivyo msimu huu, Nabi amefuta mapumziko ya wachezaji na tayari kikosi kipo kambini Avic Town Kigamboni jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi zijazo wakianza na mchezo ujao dhidi ya Ruvu Shooting.
