Na mwandishi wetu
Timu ya Azam FC imetua salama Ijumaa hii nchini Ethiopia ikieleza iko tayari kwa mchezo wao wa kwanza wa raundi ya awali wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bahir Dar Kenema ya nchini humo.
Azam ilianza safari yake hiyo Ijumaa hii alfajiri ikitokea Dar es Salaam na kutua Addis Ababa baada ya saa tatu za kuwa angani.
Ofisa Habari wa Azam, Hashim Ibwe ameeleza kuwa kikosi hicho kimetua na msafara wa wachezaji 33 pamoja na kiungo Yanick Bangala ambaye amerejea hivi karibuni baada ya kupona majeraha ya paja yaliyokuwa yakimsumbua.
“Timu iko katika hali nzuri na benchi la ufundi wako vizuri, kila kitu kimekaa kwa utaratibu na tutakwenda kucheza tukiwa tayari kwa mechi, hali ya hewa iko sawa haitusumbui hivyo tuko tayari kwa mapambano ya mchezo wa kwanza kuona namna gani tunakwenda katika mchezo unaofuata,” alisema Ibwe.
Azam itaumana na Kenema Jumapili hii kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, Addis Ababa unaoingiza mashabiki 25,000, mchezo utakaoanza saa 9.30 alasiri. Mechi ya marudiano ni Agosti 25, mwaka huu.