Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema klabu hiyo ina uwezo wa kuvutia wachezaji wa hadhi ya juu duniani katika dirisha la usajili majira ya kiangazi licha ya utata uliopo kuhusu mmiliki mpya wa klabu.
Man United imejikuta katika mjadala kuhusu kuwa na mmiliki mpya jambo ambalo linaibua wasiwasi kuhusu hatma ya klabu hiyo na mipango ya mmiliki mpya itakavyokuwa.
Akizungumzia suala hilo, Ten Hag alisema mara baada ya kukabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita, kulikuwa na ugumu kumshawishi mchezaji kujiunga Man United.
“Naiona tofauti kubwa nikilinganisha na msimu uliopita, kwa sasa wachezaji wengi wanaona maendeleo ya hapa, wanavutiwa na kila kitu, mchanganyiko na wanashawishika na kinachoendelea,” alisema Ten Hag.
Majira ya kiangazi mwaka jana kiungo, Casemiro alijiunga na timu hiyo akitokea Real Madrid kwa ada ya Pauni 70 milioni, mwingine aliyesajiliwa ni kiungo Christian Eriksen, mshambuliaji Antony na mabeki Lisandro Martinez na Tyrell Malacia.
Mwingine aliyekuwa akiwindwa na timu hiyo ni mshambuliaji Mholanzi, Cody Gakpo akitokea PSV ambaye hata hivyo baadaye aliamua kujiunga na Liverpool.
“Mwaka jana kulikuwa na wasiwasi kwa wachezaji wengi tuliowasiliana nao, mwaka huu wachezaji wengi wa hadhi ya juu wanataka kujiunga nasi,” alisema Ten Hag.
Na ingawa mjadala wa nani atakuwa mmiliki mwenye hisa nyingi katika klabu hiyo umepamba moto, Familia la Glazer ambayo kwa sasa ndiyo inayoimiliki klabu hiyo hajataja jina la tajiri mpya wanayeamini anafaa kuwa mmiliki mpya.
Hata hivyo majina ya tajiri wa Qatar aliyewekeza kwenye mabenki, Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani na Sir Jim Ratcliffe mmilili wa makampuni ya Ineos ndiyo yanayotajwa zaidi.
Man United kwa sasa ndie kinara wa Carabao Cup, taji walilolibeba Februari mwaka huu lakini pia Juni 3 wataumana na Man City katika mechi ya fainali ya Kombe la FA, mechi ambayo pia inaweza kuwapa taji lingine la pili msimu huu.
Kimataifa Ten Hag: Mastaa wanaitaka Man United
Ten Hag: Mastaa wanaitaka Man United
Read also