Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa KMC, Abdulhamid Moallin amesema siri ya ushindi kwa timu yake katika mechi tatu mfululuzo za Ligi Kuu NBC ni wachezaji kushika mapema mbinu anazowapa katika uwanja wa mazoezi.
KMC timu ambayo ilinusurika kushuka daraja msimu uliopita, ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo msimu huu ikikusanya pointi 10 ilizozipata katika mechi tano ilizocheza mpaka sasa.
Kocha huyo alisema haikuwa kazi rahisi kupata matokeo hayo katika ligi yenye ushindani kama ya msimu huu lakini wachezaji wake wamekuwa wasikivu wazuri kwa kufanyia kazi kile anachowaelekeza wanapokuwa mazoezini.
“Siri kubwa ni uwajibikaji wa wachezaji wangu katika uwanja wa mazoezi na namna wanavyoyafanyia kazi kwa vitendo yale tunayowaelekeza lakini kingine ni usajili mzuri ambao KMC tumeufanya msimu huu ambao unaendana na ushindani uliopo kwenye ligi,” alisema Moallin.
Kocha huyo alisema pamoja na mwanzo mzuri lakini bado wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanaendelea kushinda mechi zijazo ili kuendelea kukaa kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.
Alisema walipofungwa na Yanga mabao 5-0, iliwakatisha tamaa wachezaji wake lakini yeye na wenzake wa benchi la ufundi walipambana kuwajenga kisaikolojia hatimaye wamejipanga na kufanya vizuri kwenye mechi zote zilizofuata.
Moallin aliyewahi kuifundisha Azam FC msimu uliopita ameuomba uongozi wa timu hiyo kuwa na imani naye ili atimize ndoto za timu hiyo ambazo ni kushiriki michuano ya klabu Afrika msimu ujao.