Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeweka mabango katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam yakionesha ushindi wa mabao 5-1 walioupata dhidi ya mtani wake wa jadi, Simba na tayari bango hilo limekuwa gumzo mitaani.
Timu hizo zenye utani wa jadi zilikutana Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Kuu NBC na Yanga kuibuka na ushindi huo mnono na sasa wameamua kuupamba kwa kuweka bango.
Yanga wameamua kufanya hivyo kama sehemu ya utani wa kuwakera Simba lakini pia, kuendelea kuwatangaza wadhamini wao. Miongoni mwa maeneo yaliyowekwa ni Tegeta na walitarajia kuweka sehemu tofauti pia.
Bango hilo tayari limeanza kuwa mjadala mitaani na kwenye mitandao ya kijamii kwa mashabiki wa timu hizo kutoa hoja za kupinga na kuunga mkono.
Akizungumzia mabango hayo, meneja habari na mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema sababu iliyowasukuma kufanya hivyo ni kuwakumbusha watani zao kilichotokea katika mchezo huo.
“Lengo ni kuwakumbusha watani zetu kilichotokea Novemba 5, hawatakiwi kwenda mbali, mtu anavyoweweseka hivi tunapiga kichwani, kile kilichotokea hawatakiwi kwenda mbali na kusahau.
“Tumeweka mabango Dar es Salaam kote. Kutakuwa na video za magoli ya mchezo huo yataoneshwa kwenye mabango ya matangazo,” alisema Kamwe.
Kamwe alisema wanataka Watanzania waliokuwa wamesafiri wakirudi wakutane na mabango hayo na kujua kilichotokea dhidi ya watani zao.
Alisema hicho wanachokifanya ni kuwakera Simba ili wapate hasira ya kujiandaa vizuri na mchezo ujao wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast wasije kutia aibu.
Alisema kwa upande wao pamoja na utani huo, wamedhamiria kuendelea kufanya vizuri kuleta heshima na ndio maana walianzia katika mchezo huo dhidi ya Wekundu hao.