Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Melis Medo amesema siri ya timu hiyo kuanza vizuri msimu huu ni usajili bora walioufanya pamoja na wachezaji kuzingatia kile anachowaelekeza mazoezini.
Akizungumza na GreenSports leo Jumatano, kocha huyo raia wa Marekani alisema hiyo imewarahisishia kazi yeye na msaidizi wake, Kassim Liogope kutokana na matokeo mazuri wanayoyapata.
“Siri ya kuanza kwetu msimu vizuri ni usajili bora ambao tuliufanya kwenye dirisha kubwa, wachezaji wengi tuliowasajili wanajua majukumu yao, kazi yetu kubwa na msaidizi wangu ni kuwaeleza mifumo tunayotumia katika mechi,” alisema Medo.
Medo (pichani juu) alisema mkakati mkubwa ambao wamekuja nao msimu huu ni kucheza soka la kupasiana bila kujali wanacheza na timu gani na kwa kiasi kikubwa hiyo imewasaidia kupata ushindi katika mechi nyingi walizocheza ugenini.
Alisema ingawa bado ni mapema lakini malengo yao makubwa msimu huu ni kumaliza ligi kwenye nafasi tano bora na atahakikisha wanalipambania hilo ili kuwapa furaha mabosi wao pamoja na mashabiki wa timu hiyo.
Dodoma inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC ikikusanya pointi 15 katika michezo tisa iliyocheza hadi sasa.