Na mwandishi wetu
Mshambuliaji mahiri wa Namungo FC, Reliants Lusajo (pichani) ameaga kwenye timu hiyo katika dirisha hili la usajili ili kwenda kutafuta changamoto kwingine.
Nyota huyo wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Yanga na KMC za Dar es Salaam amewaaga mashabiki wa Namungo tayari kwa ajili ya changamoto mpya.
Hadi anaondoka Namungo msimu huu Lusajo amefunga mabao mawili akiwa na Wauaji hao wa Kusini ambao wanashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC wakiwa na pointi 17.
Lusajo alisema kuwa baada ya kufanya kazi Namungo kwa zaidi ya misimu miwili anaamini kuwa ni wakati sahihi kwake kwenda kutafuta changamoto mpya mahala pengine bila ya kusema anakwenda kutua wapi.
“Napenda Kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Namungo na benchi la ufundi bila kusahau mashabiki wote wa timu ya Namungo kwa kipindi chote tulichokua pamoja.
“Ni muda wangu sasa wa kuangalia changamoto sehemu nyingine, nipende kuwatakia kila la kheri katika msimu huu wa ligi kuu, muda ukifika nitaweka wazi nitakuwa wapi,” alisema Lusajo.
