Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi amesema kikosi chake kipo tayari kupigania ushindi dhidi ya US Monastir ya Tunisia na kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga kesho Jumapili itaumana na timu hiyo ya Tunisia ikiwa ni mechi yao ya tano huku ikihitaji pointi tatu ili kufikisha pointi 10 na kuwafikia Monastir pamoja na kufuzu hatua hiyo kutoka Kundi D.
Katika kundi hilo, TP Mazembe inashika nafasi ya tatu kwa pointi tatu huku Real Bamako ya Mali ikiburuza mkia ikiwa na pointi mbili.
Nabi amefafanua leo Jumamosi kuwa walipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Monastir katika mechi ya ugenini lakini tayari wamejifunza kwa aina ya mabao waliyofungwa na wamewasoma vizuri Monastir kuelekea mtanange huo.
“Mechi yetu ya kesho ni muhimu sana kwetu sababu tukipata matokeo mazuri tunafuzu moja kwa moja robo fainali lakini mechi ni ngumu sababu Monastir hawajaja kutembea hapa, wamekuja kucheza na kutafuta matokeo maana wanahitaji kumaliza wakiwa wanaongoza kundi.
“Upande wetu tumejiandaa vizuri kwa umakini, kisaikolojia na mechi hiyo na tunataka matokeo. Tunafahamu aina ya mabao waliyotufunga mwanzo, tumejifunza zaidi, tumeona video zao, ingawa tunajua watabadilika tena lakini tumewafahamu vizuri,” alisema Nabi.
Kwa upande wake kocha wa Monastir, Darko Navic alisema wamejiandaa vizuri na wako tayari kimchezo, wakihitaji ushindi ili kuendelea kujenga kujiamini kwa timu hiyo japo watacheza kwa presha kulingana na ugumu wa mechi yenyewe.
“Kwetu matokeo ni kitu muhimu, tutahitaji matokeo kikosi kiendelee kujiamini zaidi, tumejiandaa vya kutosha na tunafahamu mechi ni ngumu kiuhalisia lakini tutacheza kawaida kwa ajili ya kuitazama zaidi robo fainali,” alisema Navic.
Katika mechi nne za awali, Yanga ilipoteza dhidi ya Monastir kabla ya kuifunga Mazembe mabao 3-1 kisha ikatoka sare ya 1-1 na Bamako kabla ya kuichapa mabao 2-0 kwenye mechi ya marudiano.