Ankaragucu, Uturuki
Shirikisho la Soka Uturuki (TFF) limesimamisha mechi zote za ligi nchini humo baada ya rais wa klabu ya Ankaragucu, Faruk Koca kumchapa ngumi ya usoni mwamuzi wa mechi yao ya Super Ligi dhidi ya Rizespor.
Katika mechi hiyo iliyochezwa jana Jumatatu na kuisha kwa sare ya bao 1-1, Koca aliingia uwanjani baada ya mwamuzi kumaliza mchezo na kumpiga ngumi mwamuzi kwa kinachoamika kuwa ni kutoridhishwa na bao la kusawazisha la Rizespor lililofungwa dakika ya 97.
Picha za kwenye mitandao zimetapakaa sehemu mbalimbali zikimuonesha kiongozi huyo akiingia uwanjani na kumpiga mwamuzi katika mechi ambayo Ankaragucu walikuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Eryaman.
Baada ya tukio hilo mashabiki wa Ankaragucu nao walivamia uwanja na mwamuzi huyo, Halil Umut kujikuta akipigwa mateke na baadhi ya mashabiki hao.

Mwamuzi huyo hata hivyo baadaye aliweza kuondoka na kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa msaada wa polisi waliokuwa uwanjani hapo.
Baadaye mwamuzi huyo alipelekwa hospitali na kutibiwa majeraha aliyoyapata kutokana na kipigo na taarifa ya hospitali ilieleza kuwa licha ya kipigo lakini hakuna tishio la uhai kwa mwamuzi huyo.
“Shirikisho la Soka Uturuki limeamua kusimamisha mechi zote za ligi mara moja, klabu husika, mwenyekiti wa klabu, maofisa wa klabu na wote watakaobainika kuhusika kumvamia mwamuzi watapewa adhabu kali kadri iwezekanavyo,” ilieleza taarifa ya TFF.
Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya ameagiza kukamatwa kwa Koca na tayari watu wengine wawili wamekamatwa kwa ajili ya uchunguzi wa kipolisi kuhusiana na tukio hilo.
“Soka la Uturuki ‘limepigwa’ usiku huu wa aibu, kila aliyehusika atapata malipo yake,” alisema mwenyekiti wa TFF, Mehmet Buyukeksi.
Tukio la kupigwa kwa mwamuzi huyo mwenye beji ya Fifa tangu mwaka 2017, pia limemgusa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ambaye ametumia mitandao ya kijamii kuonesha hisia zake.
“Michezo maana yake ni amani na udugu, michezo haiendani na vurugu, katu hatuwezi kuruhusu vurugu kwenye michezo nchini Uturuki,” alisema Rais Erdogan.
