Na Hassan Kingu
Erling Haaland, mbali na kipaji, ana sifa zote za kumfanya avunje kila rekodi ya mabao iliyo mbele yake, ana kimo cha kuitumia vyema mipira ya juu, nguvu za kufumua mashuti umbali wowote, iwe ndani au nje ya 18, yote hayo yanabebwa na sifa ya kuwa mshambuliaji anayelijua goli, tusishangae akimaliza msimu na mabao 60 au zaidi.
Si mfungaji sana wa mabao ambayo mashabiki wa soka wanayaita ya ‘kideoni’ lakini ni mshambuliaji ambaye anapokuwa na mpira anajua nini akifanye ili nyavu zitikisike, sifa ambayo wachezaji wenzake wanaijua na wanajua wampe mipira ya namna gani na kwa wakati gani ili atupie kambani.
Kwa sasa yuko katika timu iliyokamilika kila idara, kuanzia golini hadi mbele, lakini pia ina benchi la ufundi lililokamilika likiongozwa na Pep Guardiola, kocha ambaye anajua namna nzuri ya kuipanga timu yake na kumtumia Haaland kupata matokeo.
Kwa maana hiyo haitokuwa ajabu kwa msimu huu wa 2022-23, Manchester City ikaweka rekodi ya kubeba mataji matatu muhimu (treble) yaani Ligi Kuu England (EPL), FA pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwa Haaland si tu huenda akaibuka kinara wa upachikaji mabao, bali pia anaweza akayapamba mabao hayo kwa kuvunja rekodi zilizopo na kuweka rekodi mpya.
Jumamosi hii ameendelea kuibeba Man City wakati ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Southampton, ushindi huo ambao umeiweka timu hiyo kileleni japo huenda ikawa kwa muda lakini kwa Haaland umekuwa na maana kwenye rekodi ya mabao.
Ameendelea kushika usukani katika EPL akiwa na mabao 15 katika mechi tisa za ligi hiyo lakini pia amefikisha mabao 20 katika mechi 13 za michuano yote kwa msimu huu na hapo hapo tayari ameifikia rekodi ya Kevin de Bruyne aliyekuwa mfungaji bora wa City kwa msimu wa 2021-22.
Hadi sasa Haaland anakuwa mchezaji wa pili wa Man City kufunga mabao katika mechi saba mfululizo baada ya Sergio Aguero ambaye alikuwa na rekodi hiyo mwaka 2019 lakini pia ni mchezaji wa kwanza kufunga hat trick (mabao matatu katika mechi moja) katika mechi tatu mfululizo za nyumbani za EPL, hiyo ilikuwa ni mechi dhidi ya Crystal Palace, Nottingham Forest na Man United.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Haaland ana mabao 25 katika mechi 20, mabao ambayo yanamfanya aivunje rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Ruud van Nistelrooy na Roberto Soldado ambao walifunga mabao 16 katika mechi zao 20 za mwanzo za michuano hiyo.
Kuna rekodi ya mabao 34 ya EPL iliyowekwa na Andy Cole msimu wa 1993-94 na Alan Shearer msimu wa 1994-95 wakati mechi za ligi zikiwa 42, hadi sasa Haaland anahitaji mabao 20 tu ili aivunje rekodi ya magwiji hao. Pia ipo rekodi ya mabao 32 ya Mohamed Salah wa Liverpool msimu wa 2017-18 katika mechi 38 za ligi. Ni suala la muda tu, Haaland ameshaonyesha kila dalili za kuvunja rekodi zote hizo.
Si tu kwamba atavunja rekodi hizo na nyinginezo bali hadi msimu wa 2022/23 utakapomalizika, kwa kasi anayoionyesha, Haaland anaweza au ana kila sababu si tu za kuvunja rekodi zilizopo bali kuja na rekodi mpya kwani kwa mabao aliyofikisha hadi sasa tusishangae akimaliza msimu na mabao 60 au zaidi.
Anahitaji kuendelea na kasi hiyo ili kuweka historia ingawa pia tusisahau kwamba yapo yanayoweza kumkwaza ikiwamo kuwa majeruhi au makocha kuwapa mabeki na timu kwa ujumla mbinu sahihi za kumdhibiti na kumpunguza kasi.
Kimataifa Tusishangae Haaland akifikisha mabao 60
Tusishangae Haaland akifikisha mabao 60
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
