Na mwandishi wetu
Mambo magumu kwa Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Esperance ya Tunisia katika mechi iliyochezwa Jumapili Januari mosi, 2026 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kupoteza kwa kiasi kikubwa matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Simba hadi sasa inashikilia mkia katika kundi lake ikiwa na pointi moja, Esperance inashika nafasi ya pili na pointi zake sita na Petro Atlético ya tatu ikiwa na pointi tano wakati Stade Malien ndiye kinara wa kundi hilo akiwa na pointi nane.
Mazingira ya kundi hilo yanaonesha kuwa Simba ikishinda mechi mbili zilizobaki itafikisha pointi saba kwa hiyo ili iweze kusonga mbele itahitaji Esperance na Petro Atlético zipoteze mechi zao mbili zilizobaki au kila moja ipoteze moja na moja iishe kwa sare.
Kwa maana nyingine Simba si tu inatakiwa kushinda mechi zilizobaki bali ishinde kwa mabao mengi lakini pia ile dhana ya adui yako muombee njaa nayo pia imebeba hatma ya Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa 2025-26.
Kilichoifikisha Simba katika hali hiyo ni mechi yao na Esperance, mechi ambayo ilitoa matumaini ya timu hiyo kupata ushindi kabla ya mambo kuharibika na kujikuta wakitoa sare ya 2-2 huku Esperance wakikosa penalti.
Simba iliuanza mchezo huo vizuri na kuonesha kila dalili za kutoka uwanjani na pointi tatu baada ya kupata bao la kwanza dakika ya 39 lililofungwa na Shomari Kapombe.
Shamrashamra za mashabiki wa Simba baada ya bao hilo ziliongezeka kwa mara ya pili baada ya Yusuph Kagoma kuongeza bao la pili katika dakika za nyongeza kabla ya timu kwenda mapumziko.
Mambo yalianza kuiendea kombo Simba katika dakika ya 64 baada ya Aboubacar Diakité kuipatia Esperance bao la kwanza kabla Kouceila Boualia hajasawazisha dakika 15 baadaye na kuwaacha mashabiki wa Simba vichwa chini.
Kama hiyo haitoshi mashabiki hao waliingia unyonge tena katika dakika za nyongeza baada ya Esperance kupata penalti lakini Hamza Jelassi alishindwa kuitumia penalti hiyo kuipatia Esperance bao.
Katika mechi zijazo Simba itakuwa ugenini Angola kuumana na Petro de Luanda wakati Esperance itasafiri hadi Mali kuikabili Stade Malien.
Kimataifa Esperance yaiweka pagumu Simba
Esperance yaiweka pagumu Simba
Read also
