Barcelona, Hispania
Klabu ya Barcelona ‘Barca’ imemtaka mtendaji mkuu wa Ligi Kuu Hispania au La Liga, Javier Tebas ajiuzulu kwa kutoa ushahidi wa uwongo kwa klabu hiyo kuhusu tuhuma za kutoa rushwa kwa mwamuzi.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, Tebas anadaiwa kuwasilisha ushahidi wa maandishi kwa waendesha mashitaka akiwataja marais wa zamani wa Barca katika kashfa hiyo.
Tebas amewahusisha marais hao na kashfa inayoiandama klabu hiyo ikidaiwa kumhonga makamu rais wa zamani wa kamati ya waamuzi Hispania kwa kinachodhaniwa kuwa ni kutaka upendeleo.
Habari za ndani hata hivyo zinadai kwamba ushahidi uliowasilishwa na Tebas dhidi ya marais hao, Sandro Rosell na Josep Maria Bartomeu hauhusiani na kashfa iliyopo.
Akijibu madai ya Barca kupitia akaunti ya Twitter, Tebas alisema kichwa cha habari cha nakala hiyo kilikosewa kwani hakumtuhumu yeyote kwa lolote na anamtuhumu mwandishi kwa madai ya upotoshaji.
Barca hata hivyo wametaka ufafanuzi wa kina kutoka kwa Tebas na kuelezea hasira zao na namna walivyochukizwa na jambo hilo wakimtaka Tebas ajiuzulu.
“Barcelona, kama alivyosema hivi karibuni rais Joan Laporta imejikuta katika mkakati maalum wa kuchafuliwa na vyombo vya habari kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni, Barca haikuwahi kununua mwamuzi,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
“Si mara ya kwanza Rais wa La Liga amekuwa akitumia silaha yake ya vyombo vya habari kuichafua Barcelona lakini ukiacha upuuzi wake uliozoeleka hatukuwahi kufikiria angetaraji kuidhalilisha klabu yetu na ushahidi wa uwongo,” ilieleza taarifa ya Barca.
Baada ya waendesha mashitaka kuwasilisha tuhuma, mahakama nchini Hispania inachunguza malipo ya Euro 7 milioni ambayo Barca iliyafanya kwa rais wa zamani wa kamati ya waamuzi Hispania, Jose Maria Negreira kati ya mwaka 2001 na 2018.
Wakati ikidhaniwa kwamba malipo hayo yalitolewa ili klabu hiyo ipendelewe katika mechi zao, Barca imekana jambo hilo ikidai kwamba ilimlipa Negreira na kampuni yake ili awasaidie kupata taarifa ya ufundi kuhusu waamuzi na mwenendo wa mechi zao.