Rio de Janeiro, Brazil
Wananchi wa Brazil, jana Ijumaa wamefanya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha gwiji wa soka duniani, Pele ambaye alifariki dunia kwa maradhi ya saratani akiwa na miaka 82.
Pele ambaye anashikilia rekodi ya kubeba Kombe la Dunia mara tatu akiwa na timu ya taifa ya Brazil, alifariki mwaka jana, kifo ambacho kiliteka hisia za mashabiki wa soka duniani kote.
Katika hafla iliyofanyika leo mjini Rio de Janeiro, picha na mabango ya gwiji huyo yalionekana ikiwamo picha yenye jezi namba 10 yenye jina la Pele katika bango maalum lililokuwa na ujumbe wa Papa Francis uliosomeka, ‘Pele alikuwa muumini wa kweli Mkatoliki katika maisha yake yote.’
Hafla nyingine za kidini zilifanyika Santos, mji ambao Pele aliweka rekodi ya kuvutia ya mabao akiwa na timu ya Santos pamoja na kwenye mji mdogo wa Tres Coracoes, mji ambao Pele alizaliwa mwaka 1940.
Klabu ya Santos nayo ilifanya hafla ndogo kwenye Uwanja wa Vila Belmiro unaotumiwa na klabu hiyo ambapo mmoja wa watoto wa Pele, Edson Cholbi do Nacimento, alirusha juu mabaluni 10 ya rangi nyeupe akiwa katikati ya uwanja.
Nalo Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lilituma ujumbe maalum wa video ambayo ilikuwa na baadhi ya matukio ya Pele yakiandamana na ujumbe uliosomeka, “Kumbukumbu ya Pele itaendelea kudumu.”
Mapema mwaka huu kamusi ya Brazil ilimuenzi gwiji huyo kwa kuliweka jina la Pele katika kamusi hiyo, jina hilo likiwa na maana ya mtu aliyefanya mambo makubwa, ya kipekee na yasiyo na mfano.
Katika maisha yake ya soka, Pele amejipatia umaarufu akiwa na timu ya taifa ya Brazil akiwa na rekodi ya kubeba Kombe la Dunia mara tatu pamoja na klabu ya Santos ambayo aliipatia mafanikio lukuki.
Kimataifa Brazil waadhimisha mwaka mmoja wa kifo cha Pele
Brazil waadhimisha mwaka mmoja wa kifo cha Pele
Read also