Na mwandishi wetu
Licha ya mshambuliaji wa Simba, Moses Phiri kuonekana kutotumika kwenye kikosi cha timu hiyo hivi karibuni, kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema bado anamhitaji mchezaji huyo kuelekea msimu ujao.
Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao 10 msimu huu kwenye Ligi Kuu NBC, amekuwa akisota benchi tangu ujio wa Robertinho raia wa Brazil na kuibua hisia pengine anaweza kuachwa kwenye dirisha kubwa la usajili.
Meneja Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa Robertinho bado anahitaji huduma ya mshambuliaji huyo na hiyo ni kutokana na rekodi zake nzuri za mabao alizokuwa nazo msimu huu.
“Sababu ya Robertinho kutompa nafasi Phiri ni kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu aliyoyapata lakini rekodi zake zimemshawishi kocha kutaka kufanya naye kazi msimu ujao akiamini atakuwa fiti kwa ajili ya mapambano,” alisema Ally.
Ally alisema anatambua timu hiyo ina mpango wa kukiboresha kikosi chao kwa kusajili washambuliaji wa nguvu lakini hiyo itakuwa ni kipimo kingine kwa Phiri kumthibitishia Robertinho kuwa ni mchezaji mwenye ubora wa kuichezea Simba.
Phiri aliyejiunga na kikosi cha Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Zanaco ya kwao Zambia, mkataba wake na Simba unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao.