Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe inadaiwa amekubali kujiunga na Real Madrid mara tu baada ya mkataba wake na PSG kufikia ukomo Juni mwaka huu.
Mchezaji huyo bado hajasaini mkataba na klabu hiyo lakini kilichopo wazi ni kuwa kila kitu kinaenda vizuri na sasa ni suala la muda tu kabla ya mchezaji huyo kumwaga wino na vigogo hao wa Hispania.
Mbappe, 25, ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa, awali alinukuliwa akiwaambia mabosi wake wa PSG kwamba ana nia ya kuachana na timu hiyo baada ya msimu huu.
Inadaiwa kwamba mpango wa Real Madrid kumsajili Mbappe utatangazwa rasmi pale itakapobainika kwamba Real Madrid na PSG haziwezi kukutana kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Habari za awali zilidai kwamba Mbappe alikutana na Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi na kumwambia kwamba anataka kujiunga na Real Madrid na angependa jambo hilo liwe limekamilika kabla ya mwezi Machi mwaka huu.
Inadaiwa kwamba mshambuliaji huyo anatarajia kusaini mkataba wa miaka mitano na Real Madrid, mkataba ambao utamuwezesha kuvuna kitita cha Pauni 12.8 milioni kwa mwaka pamoja na marupurupu mengine.
Habari zaidi zinadai kwamba kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti tayari ameshapiga hesabu za namna ya kumtumia Mbappe katika eneo la ushambuliaji akiwajumuisha, kiungo wa England Jude Bellingham na mshambuliaji wa Brazil, Vinicius Junior.
Ikitokea kama kiungo Luka Modric kutoka Croatia ataihama timu hiyo baada ya msimu huu, inadaiwa kwamba Mbappe atakabidhiwa jezi namba 10 ambayo kwa sasa inavaliwa na Modric.
Kimataifa Mbappe, Real Madrid ni suala la muda tu
Mbappe, Real Madrid ni suala la muda tu
Read also