Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kikosi chake kipo tayari na kamili kuivaa Somalia kesho wakitarajia kupiga soka safi na ushindi katika mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Huo ni mchezo wa pili baina ya timu hizo kuwania kufuzu kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) inayotarajia kufanyika Algeria, mwakani.
Katika mechi ya awali, Stars iliifunga Somalia kwa bao 1-0 iliyokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkapa, wakiutumia uwanja huo kikanuni kutokana na sababu za kiusalama nyumbani kwao.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Poulsen alisema baada ya mazoezi ya kimbinu kwa kila nafasi, sasa kinachobaki ni ubora wa wachezaji hao kuamua matokeo huku akiweka wazi kumkosa kipa, Aishi Manula kutokana na majeraha.
“Wachezaji wote wako tayari kwa ajili ya mechi kasoro Aishi kwa sababu alipata majeraha kwenye mechi ya mwisho lakini kiujumla wachezaji wamejiandaa vya kutosha kwa maana ya mazoezi tuliyokuwa tukifanya kwenye nafasi zote tatu.
“Kuanzia washambuliaji namna ya kushambulia tunapofika kwenye eneo la mwisho la adui, jinsi ya kutengeneza nafasi na kutembea na mpira kwa wa kati, na mwisho wa siku baada ya yote kama kocha nasubiri maamuzi na ubora kutoka kwao ndiyo yatupe matokeo.
“Tumefanya pia kwa viungo namna ya kutengeneza nafasi nyingi zaidi zitakazotupa mabao na pia mabeki kutoruhusu kutoa nafasi kwa wapinzani kama ilivyokuwa mara ya mwisho tuliwapa nafasi nyingi, tunataka kupiga pasi safari hii na kuutembeza mpira, hiyo ndiyo falsafa yetu,” alisema Poulsen.
Katika mchezo huo, Stars inahitaji sare yoyote au ushindi ili kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ili kujihakikishia nafasi nzuri ya kufuzu michuano hiyo.
Mshindi wa jumla wa mchezo huo atacheza na Uganda ambao utakuwa mchujo wa mwisho wa kuwania kufuzu Chan inayotarajia kuanza kuunguruma mwezi Januari hadi Februari, mwakani.
Kimataifa Kim: Tupo tayari kuivaa Somalia
Kim: Tupo tayari kuivaa Somalia
Read also