Munich, Ujerumani
Rais wa heshima wa klabu ya Bayern Munich, Uli Hoeness amesema klabu hiyo inashindana na Liverpool kuisaka huduma ya kocha Xabi Alonso ambaye kwa sasa anainoa Bayer Leverkusen.
Alonso ambaye amewahi kuzichezea timu hizo mbili kwa nyakati tofauti, amekuwa na mafanikio tangu aanze kuinoa Leverkusena na kwa msimu huu timu hiyo inaelekea kutwaa taji la Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga.
Bayern na Liverpool baada ya msimu huu kila moja inatarajiwa kuwa na kocha mpya kwa kuwa makocha wao wa sasa hawatoendelea na timu hizo baada ya kufikia makubaliano.
Jurgen Klopp wa Liverpool tayari amekubaliana na uongozi wa klabu hiyo kuwa hatoendelea na timu hiyo kwa msimu ujao wakati Thomas Tuchel na Bayern nao pia wamekubaliana kuachana baada ya msimu huu.
Hoeness alifafanua kwamba klabu kama Liverpool, Real Madrid, Leverkusen na Bayern zote zinaweza kufanyia kazi suala la kumuajiri kocha huyo kwa kile ambacho tayari amekionesha.
“Amethibitisha kwamba anaweza kuinoa timu kubwa, kwa sasa ni kama vile hakuna kocha ambaye anaweza kujadiliwa na yuko huru au ambaye hana kazi au yuko katika mapumziko,” alisema Hoeness.
Mkataba wa Alonso na Leverkusen unafikia mwisho mwaka 2026 wakati kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti naye mkataba wake na klabu hiyo unafikia mwisho kipindi hicho hicho.
Kwa hiyo si Liverpool na Bayern pekee ambazo zinaweza kuingia vitani kusaka huduma ya Alonso bali pia Real Madrid, timu ambayo pia aliwahi kuichezea miaka ya nyuma.