Na mwandishi wetu
Simba, Azam FC zimeanza vyema michuano ya klabu inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ushindi, Simba ikiilaza Gaborone United ya Botswana bao 1-0 na Azam ikiibugiza El Mereikh Bentiu ya Sudan Kusini mabao 2-0.
Katika ushindi, huo uliopatikana Jumamosi hii Septemba 20, 2025, Simba na Azam zote zilitamba ugenini, Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa Gaborone, Botswana wakati Azam inayopambana kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa Juba, Sudan Kusini.
Simba waliandika bao hilo pekee na la ushindi katika dakika ya 16 mfungaji akiwa Elly Mpanzu ambaye alifunga kwa kichwa akitumia vizuri krosi ya beki na nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe.
Ushindi huo unaiweka Simba katika nafasi nzuri kwa mechi ya marudiano ambayo itachezwa mwishoni mwa wiki ijayo jijini Dar es Salaam ambapo mshindi wa jumla ataumana na mshindi wa mechi kati ya Nsingizini ya Eswatini na Simba Bhora ya Zimbabwe.
Nayo Azam ikiwa Uwanja wa Taifa Juba ilipata ushindi huo kwa mabao ya Feisal Salum au Fei Toto ambaye alifunga bao la kwanza dakika ya 21 baada ya kuufumania mpira na kufumua shuti lililomshinda kipa wa El Mereikh, Monged Elneel.
Azam waliongeza bao la pili dakika ya 68 lililofungwa na Jephte Kitambala akimalizia kwa kuujaza wavuni mpira ulioanzia kwa Baraket Lhimid.
Baada ya ushindi huo Azam wanasubiri kurudiana na timu hiyo jijini Dar es Salaam ambapo mshindi wa jumla atakuwa na kibarua katika hatua inayofuata dhidi ya KMKM au AS Port.
Wakati Simba na Azam zikifurahia ushindi wa ugenini, mambo hayakuwa mazuri kwa Mlandege ya Zanzibar kwenye Ligi ya Mabingwa baada ya kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Ethiopia Insurance.
Matokeo hayo ya ugenini yanawaweka Mlandege katika wakati mgumu kwenye mechi ya marudiano ambayo itapigwa wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar ambapo mshindi wa jumla ataumana na APR ya Rwanda au Pyramids ya Misri.
Kimataifa Simba, Azam zatamba CAF
Simba, Azam zatamba CAF
Read also
