Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ amesema timu yake imepania kuonesha soka safi la kuwaburudisha wananchi wa Kigoma na kuwapa matokeo ya ushindi kesho Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu NBC dhidi ya Yanga.
Baresi ameeleza hayo leo Jumamosi alipokuwa akihojiwa na GreenSports kuelekea mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma nyumbani kwa Mashujaa kuanzia saa 10 jioni.
Akifafanua kuhusu maandalizi yao alisema pamoja na kujiandaa vyema lakini pia wamewaeleza wachezaji wao nini cha kufanya kutokana na wachezaji wanaokutana nao.
Alisema kwamba wengi wao ni wajanja wa kuhukumu yanapopatikana makosa hivyo wamewaeleza wachezaji nini cha kufanya kuepuka hayo na hatimaye kuvuna pointi tatu.
“Tunatambua wana mchezaji mmoja mmoja ambao muda mwingi unapofanya makosa wanaweza kukuhukumu na kuamua matokeo, kwa hiyo katika hilo wachezaji wetu tushawafundisha na tumewahimiza sana tuwe na hali ya tahadhari ya kucheza na wachezaji wa namna hiyo.
“Kwa hiyo kwa kifupi niseme wazi kwamba litakuwa pambano la kuheshimisha mkoa wa Kigoma na wananchi wake ambao wanahitaji kuona timu yao inabaki ligi kuu haishuki, sasa inabaki kwa staili gani?
“Ni kupata pointi tatu kwenye kila mchezo tunaocheza na sio Yanga tu, kila mchezo utakaofuata na kesho tunataka alama tatu kuhakikisha tunakaa vizuri, ikishindkana hivyo basi tusipoteze huu mchezo,” alisema Baresi.