Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeingia mkataba wa Sh milioni 40 na mashirika mawili tofauti ya ZIPA na ZRA ya Visiwani Zanzibar ambapo hafla hiyo ya utiliaji saini imefanyika leo Jumatatu visiwani Zanzibar.
Hafla hiyo pia imekwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya Ibrahim Abdallah ‘Bacca Day’ ambayo kilele chake itakuwa Desemba 2, mwaka huu kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba hiyo, Rais wa Yanga, Hersi Saidi alisema wameamua kushirikiana na makampuni hayo ili kuongeza mapato yatakayosaidia katika kipindi hiki ambacho timu inatumia gharama kubwa katika safari na maandalizi ya timu.
“Tumechagua Zanzibar kuzindua Bacca Day, sababu ni mwenyeji wa hapa, lakini tumetumia tukio hili kuongeza mapato kwa klabu yetu, kwa kusaini mikataba na Zanzibar Investment Promotion Authority (ZIPA) wenye thamani ya Milioni 20 pamoja na Zanzibar Revenue Authority (ZRA) wenye thamani ya milioni 20 kwa siku saba pekee,” alisema Hersi.
Naye Mkurugenzi wa ZIPA, Alhaji Jecha alisema hakujifikiria mara mbili baada ya kuelezwa mpango wa kushirikiana na Yanga na hiyo ni kutokana na ukubwa wa klabu hiyo na mafanikio iliyonayo ndani ya uwanja.
“Nilipoletewa mpango wa kushirikiana na Yanga, nikauliza hii si ndio ile timu ya Wananchi? Nikajibiwa ndio, nikasema hilo limepita sababu niliamini wana uwezo wa kuturusha kwa jamii na kutangaza bidhaa zetu kwa mafanikio zaidi,” alisema Jecha.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa ZRA, Shaban Ramadhani alisema wamechagua kufanya kazi na klabu hiyo ya Wananchi sababu ni ‘Taifa Kubwa’ na taarifa zote zinazoihusu timu hiyo lazima itetemeshe vichwa vya watu.
“Nani ambaye hataki kuonja tone hili la ukubwa wa Yanga, ZRA tulikuwa tunalitamani sasa limekuja hatuwezi kuliachia likapita,” alisema Ramadhani.
Kuhusu Bacca Day, Hersi alisema Bacca ni mmoja wa wachezaji walioonesha juhudi kubwa kwani tangu ajiunge na timu hiyo kiwango chake kimezidi kuimarika na kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji wakutumainiwa kwenye kikosi chao na timu ya taifa ya Tanzania.
Katika michezo ya hatua ya awali Yanga ilitambulisha Max Day na Aziz Ki Day ambapo safari hii wamekuja na Bacca Day ambayo uzinduzi wake umefanyika kwao Zanzibar.