Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imeachana na kocha wake mkuu, Roberto Oliviera au Robertinho ikiwa ni siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 5-1 na mahasimu wao Yanga katika mechi ya Ligi Kuu NBC.
Simba imechukua uamuzi huo baada ya kukaa na kocha huyo na kufikia muafaka wa kuvunja mkataba na sasa timu hiyo itakuwa chini ya Daniel Cadena atakayesaidiwa na Suleiman Matola.
Taarifa ya Simba iliyopatikana leo Jumanne haikutaja sababu za kufikia uamuzi huo ingawa inaeleweka kwamba kipigo cha Yanga ndicho kilichoufanya uongozi kuachana na kocha huyo kutoka Brazil.
Robertinho aliyejiunga na Simba takriban miezi 10 iliyopita ameachwa na Simba akijivunia kuipa timu hiyo taji la Ngao ya Jamii lakini pia ameifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Taarifa ya klabu ya Simba ilifafanua kuwa mchakato wa kumsaka mrithi wa kocha huyo unaendelea na utakamilika katika siku za karibuni.
Sambamba na Robertinho, Simba pia imeamua kuachana na kocha wa viungo, Corneilo Hategimana na kama ilivyo kwa Robertinho sababu za kuachana na kocha huyo pia hazijawekwa wazi.
Tangu Simba ifungwa na Yanga juzi Jumapili fununu za kutimuliwa kwa kocha huyo zilianza kuibuka na hata kabla ya hapo baadhi ya mashabiki walidai kutofurahishwa na uchezaji wa timu hiyo licha ya ushindi ambao wamekuwa wakiupata katika mechi walizocheza.
Soka Simba yamfuta kazi Robertinho
Simba yamfuta kazi Robertinho
Read also