London, England
Mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Son Heung-Min (pichani) ameelezea dhamira yake ya kuendelea kuichezea timu hiyo licha ya kupata ofa nono ya kujiunga na klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia.
Habari zilizopatikana jana Jumatatu zilieleza kuwa Son alikuwa akiwindwa na klabu ya Al-Ittihad iliyokuwa tayari kumpa mkataba wa miaka minne utakaokuwa na thamani ya Dola 32.8 milioni kwa kila msimu.
Wakati mabosi Al-Ittihad wakiwa na matumaini makubwa ya kumpata mchezaji huyo, Spurs inadaiwa haipo tayari kusikiliza ofa yoyote kwa mchezaji huyo raia wa Korea Kusini.
Son mwenyewe naye aliamua kuvunja ukimya hii leo aliposisitiza kwamba dhamira yake ni kuendelea kuichezea Spurs inayoshiriki Ligi Kuu England.
Mchezaji huyo alizungumza na mwandishi mmoja na kusisitiza kwamba bado ana mambo anayotaka kuyatimiza katika Ligi Kuu England na ndicho kitu pekee anchokipa umuhimu kwa wakati huu.
“Nina mengi ya kufanya katika ligi kuu, sijali kuhusu pesa kwa wakati huu na ufahari wa kucheza soka, badala yake kucheza katika ligi niipendayo ndilo jambo muhimu, nataka kucheza zaidi kwa ajili ya Tottenham, nitajiandaa vizuri nikirudi Spurs,” alisema Son.
Habari nyingine hata hivyo zinadai kwamba Son mwenye mkataba na Spurs hadi mwaka 2025 huenda akashawishika kujiunga na Al-Ittihad ambayo tayari imeshamsajili mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema huku wakidaiwa kuwa mbioni kukamilisha usajili wa kiungo wa Chelsea, N’Golo Kante.