Berlin, Ujerumani
Shirikisho la Soka Ujerumani (DFB) lipo mbioni kufanya mazungumzo na Jurgen Klopp ili awe kocha mkuu wa timu ya taifa baada ya kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia na Julian Nagelsmann kung’atuka.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na hoja miongoni mwa mashabiki kumtaka kocha huyo wa zamani wa Liverpool akabidhiwe timu hiyo jambo ambalo DFB imeliafiki na inajiandaa kwa hilo.
DFB imedai kuwa itaandaa utaratibu wa kufanya mazungumzo na Klopp ambaye pia anaonekana yupo tayari kwa jukumu hilo baada ya kuvunja mkataba na Nagelsmann, kocha wa zamani wa Bayern Munich.
Nagelsmann, 38, ameshindwa kuiongoza Ujerumani kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea katika nchi za Marekani, Mexico na Canada ambapo Jumatatu iliyopita timu hiyo ilitolewa katika hatua ya 32 bora baada ya kufungwa na Paraguay katika penalti.
Baada ya Ujerumani kutolewa, Nageslmann hakuonesha dalili zozote za kuachana na timu hiyo yenye rekodi ya kutwaa ubingwa wa dunia mara nne, badala yake alisema yeye si mtu anayekimbia.
Kocha huyo ambaye aliteuliwa kuiongoza timu hiyo mwaka 2023 hata hivyo, Ijumaa Julai 3, 2026 alikuja na kauli tofauti akidai amefikiria tofauti baada ya kufanya mazungumzo binafsi na watu mbalimbali.
“Nimefanya tafakuri ya kina katika siku hizi tangu tutolewe na nimewasiliana na watu binafsi ninao waamini pamoja na walio ndani ya shirikisho,” alisema Nagelsmann.
Haya ni mashindano ya pili makubwa kwa Nageslmann ambaye mwaka 2024 aliiongoza timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Ulaya (Euro 2024) na kutolewa katika hatua ya robo fainali ikishindwa kutamba mbele ya Hispania ambao baadaye waliibuka mabingwa.
