Na mwandishi wetu
Mshambuliaji mpya wa Simba, Dejan Georgijevic amesema kwamba hakuwahi kuwa na presha kabla ya kufunga bao lake la kwanza jana kwa kuwa anafahamu ubora wake hivyo alijua ni suala la muda tu na si vinginevyo.
Dejan raia wa Serbia ameifungia Simba bao hilo kwenye ushindi wa mabao 2-0 walioupata dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam baada ya safu ya ulinzi ya Kagera kujichanganya na Dejan kuuweka sawa mpira huo kabla ya kutupia wavuni.
Kabla ya bao hilo, Dejan ambaye amekuwa akivuma kwa jina la Mzungu alikuwa akikosolewa kuwa hana lolote baada ya kuingia akitokea benchi kwenye mechi mbili za ushindani zilizopita bila ya kufunga bao huku mashabiki wa Wekundu hao wakitegemea makubwa zaidi kutoka kwake hasa baada ya kuondoka kwa Meddie Kagere na Chris Mugalu kwenye timu hiyo.
“Nimefurahi kufunga bao leo (jana) najua mashabiki wamefurahi na nilikuwa nikiona jumbe zao za kuhitaji nifanye hivyo na nimefurahi tumepata ushindi.
“Niseme tu sikuwahi kuwa na presha kabla kisa sijafunga bao na zaidi nilitumia kama dakika 20 tu katika kila mchezo na kwa sababu nafahamu ubora nilionao sikuwa na wasiwasi kabisa na hilo na nitazidi kucheza kwa uwezo wangu wote na kujitoa kwa asilimia 100 kuhakikisha tunapata ushindi kila mechi,” alisema Dejan.
Simba sasa inaongoza ligi baada ya mechi mbili za awali za Ligi Kuu ya NBC iliyoanza katikati ya wiki hii. Wekundu hao wana alama sita na mabao matano ya kufungwa, ikiwa ndiyo timu pekee ambayo imecheza mechi mbili bila kuruhusu kufungwa bao mpaka sasa.
Soka Dejan: Sijawahi kuwa na presha Simba
Dejan: Sijawahi kuwa na presha Simba
Read also