Na mwandishi wetu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro (pichani) ameupongeza uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuingia mkataba wa miaka mitano na Kampuni ya Sandaland Fashion Wear wenye thamani ya Sh bilioni 3 kwa ajili ya kuzivalisha timu zote za taifa.
Pongezi hizo zimetolewa baada ya kukamilika kwa zoezi la utiaji saini wa mkataba huo uliofanyika kwenye hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Nashukuru sana uongozi wa TFF chini ya uongozi wa ndugu yangu, Wallace Karia ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, TFF inaingia mkataba na mtengenezaji jezi kwa ajili ya timu zote za taifa, tunaweza kulichukulia jambo hilo kama dogo sana lakini halijawahi kufanyika na linafanywa na TFF chini ya jemedari Wallace Karia.
“Nasisitiza haya kwa sababu sisi Watanzania ni wazuri sana wa kukosoa lakini tunakuwa wachoyo kusifia pale jambo zuri linapofanyika, ili timu zote za taifa zipate jezi rasmi zinazotengenezwa na kampuni yenye heshima kubwa hapa Tanzania,” alisema Ndumbaro.
Aidha, imebainishwa katika mkataba huo TFF itakuwa ikipata jezi na pia sehemu ya fedha kwa ajili ya timu zote za soka za taifa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Sandaland, Yusuph Yenga alisema kampuni hiyo ina uzoefu wa kutengeneza jezi na kuahidi kuwa jezi hizo zitakuwa na ubora na viwango vya hali ya juu.