Na mwandishi wetu
Bondia Hassan Mwakinyo ‘Champez’ amesema anashukuru kupata nafasi ya kupigana na bondia bora Afrika, Patrick Alotey raia wa Ghana huku akiamini atafanya vyema na mpinzani wake atakwenda kusimulia kitakachomtokea siku hiyo.
Mwakinyo amezungumza hayo leo Jumatano jijini Dares Salaam kuelekea pambano hilo ambalo atakuwa akitetea mkanda wake wa WBO, litakalopigwa Mei 31 mwaka huu, Masaki jijini Dar es Salaam.
“Kwanza niwashukuru makocha wangu, mashabiki wangu ambao wameendelea kunitumainia hata baada ya kupita kipindi kirefu, ila kumekuwa na maneno mengi ya kimichezo lakini nafikiri hili pambano la tarehe 31 kwangu mimi litakwenda kudhihirisha ukweli unazoungumzwa na watu wazuri na wabya juu yangu kwamba mimi ni nani.
“Kwangu mimi kupigana na bondia mwenye rekodi kubwa Afrika ni bahati kwenye maisha yangu, ‘boxer’ mwenye rekodi kubwa kidunia, hajawahi kupigwa na Mwafrika, lakini mimi nitakuwa Mtanzania, Mwafrika wa kwanza kuharibu rekodi ya bondia Alotey.
“Naomba tu listokee jambo la kinchi likasababisha pambano kuahirishwa lakini nina uhakika asilimia 100 atakwenda kusimulia kitakachomtokea,” alisema Mwakinyo.
Wakati huohuo, katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Kampuni ya Golden Boy Promotion, Shomari Kimbau alimtaka mwanamuziki, Rajabu Kahali kufuata taratibu rasmi za ngumi kama kweli anataka kupambana na Mwakinyo ulingoni.
Kimbau alisema kwamba anaamini Mwakinyo ana uwezo wa kumchapa Harmonize hata akiwa amefungwa mkono mmoja.
Kimbau amezungumza hayo baada ya hivi karibuni kuibuka malumbano na kejeli mitandaoni baina ya wawili hao kabla ya majuzi kusambaa video inayowaonesha Mwakinyo na Harmonize wakizuiwa ili wasipigane.
Tukio hilo lilitokea wawili hao walipokutana kwenye gym moja jijini Dar es Salaam na kuanza kurushiana maneno kila mmoja akimtambia mwenzake kwamba anaweza kupigana na mwenzake na kumpiga.