Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumamosi imeichapa Asas ya Djibout mabao 5-1 na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa inajiandaa kuivaa El-Mereikh ya Sudan katika hatua inayofuata.
Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo ambayo pia ilichezwa kwenye uwanja wa Azam Complex kama ilivyo leo baada ya Asas kuamua kuufanya kuwa uwanja wao wa nyumbani, Yanga ilitoka na ushindi wa mabao 2-0.
Ushindi wa leo wa Yanga ulianzia dakika ya saba ya mchezo huo kwa bao la kichwa lililofungwa na Maxi Nzengeli ambaye aliunganisha krosi ya Moloko iliyotokana na pasi ya juu ya Jonas Mkude au Nungunungu.
Dakika moja kabla ya timu kwenda mapumziko, Yanga iliandika bao la pili lililofungwa na Hafiz Konkoni kwa mpira ulioanzia kwa pasi ya juu iliyopigwa kiufundi na Salum Aboubakar au Birthday Boy kama alivyokuwa akiitwa leo.
Baada ya Salum Aboubakar kuupiga mpira wa juu, Stephanie Aziz Ki alipambana na lakini mpira alioupiga uliokolewa na beki wa Asas kabla ya kumkuta Konkoni ambaye aliujaza wavuni.
Yanga waliandika bao la tatu dakika 10 baada ya mapumziko, bao lililofungwa na Pacome Zouazoua ambaye alionesha juhudi binafsi kwa kumpiga chenga kipa, na beki kabla ya kumpiga tena chenga kipa na kuujaza wavuni.
Dakika ya 69 Clement Mzize aliipatia Yanga bao la nne akiunganisha kwa kichwa pasi ya Kibabage, bao ambalo liliwaamsha Asas na juhudi zao kuzaa matunda dakika ya 84 walipopata bao la penalti iliyofungwa na Tito Mayor.
Nzengeli hata hivyo aliwakatisha tamaa Asas alipoipatia Yanga bao la tano ambalo ni bao lake la pili katika mechi hiyo, akiitumia vizuri pasi ya Mzize.
Kwa ujumla Yanga iliutawala vizuri mchezo hasa kipindi cha kwanza ambapo, Asas hawakufanya shambulizi lolote la maana hali iliyomfanya kipa Djigui Diarra kutopata misukosuko ya mara kwa mara.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC, hii ni mara ya pili kutoka uwanjani na mabao matano katika siku za karibuni, ikiwa imetoka kuifunga idadi kama hiyo KMC ya Kinondoni katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu NBC.
Kimataifa Yanga yaipiga Asas Djibout 5-1
Yanga yaipiga Asas Djibout 5-1
Read also