Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amemtetea mshambuliaji wake, Erling Haaland ambaye kiungo wa zamani wa Man United, Roy Keane amemponda na kumfananisha na mchezaji wa daraja la pili katika mechi dhidi ya Arsenal.
Keane, nahodha wa zamani wa Man United alikuwa akizungumzia mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya 0-0 ambapo alisema kwa ujumla Haaland alikuwa hovyo mno mfano wa mchezaji wa daraja la pili.
“Sikubaliani naye, si kweli kabisa, Haaland ni mshambuliaji bora duniani, alitusaidia kubeba taji msimu uliopita” alisema Pep kuhusu Haaland ambaye msimu uliopita aliifungia Man City mabao 52 katika mashindano yote na msimu huu hadi sasa ana mabao 18 katika Ligi Kuu England (EPL).
“Katika soka kunakuwa na sababu zaidi ya moja, kuna wakati unakuwa na mafanikio, kuna wakati unakosa mafanikio, sababu zinakuwa nyingi na hayo ndiyo mambo ya soka, ni mchezo unaohusisha timu,” alisema Pep.
Akizungumza katika kipindi cha michezo cha Sky, Keane alisema kwamba kiwango cha Haaland kilikuwa kibaya na si kwa mechi hiyo tu ya Jumapili.
“Kwa ujumla kiwango cha uchezaji wake ni hovyo sana na si leo (Jumapili) tu, uchezaji wake kwa ujumla ni mbaya, nafikiri anatakiwa kufanya bidii katika hilo, anakuwa kama mchezaji wa daraja la pili,” alisema Keane.
Kimataifa Pep ampinga Roy Keane kuhusu Haaland
Pep ampinga Roy Keane kuhusu Haaland
Read also
