Na mwandishi wetu
Baada ya kuifungia Simba bao katika mechi ya kirafiki nchini Misri, kiungo mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Augustine Okrah ametamba kuwa atahakikisha anaifungia mabao mengi timu hiyo msimu ujao ili kuwapa raha mashabiki wao.
Okrah aliyetua Simba hivi karibuni kwa kandarasi ya miaka miwili amezungumza hayo baada ya juzi kuifungia bao Simba dhidi ya Ismaily kwenye mchezo wa kirafiki ulioisha kwa sare ya 1-1.
Akizungumzia bao lake hilo, Okrah alisema amefurahi kufungua akaunti ya mabao ndani ya timu hiyo na anashukuru kupewa nafasi hiyo na kocha wa Wekundu hao, Zoran Maki kwani pia amekuwa akimuelekeza vyema nini cha kufanya ili afunge mabao ya kutosha.
“Kiukweli kwanza namshukuru kocha kwa kunipa nafasi ya kucheza mechi hii na kufanya iwe kitu kizuri kufunga bao langu la kwanza kwa Simba. Hii ni mechi yangu ya kwanza, kuna vitu nahitaji kuimarika na kufunga mabao mengi kwa ajili ya mashabiki wa Simba.
“Ilikuwa siku nzuri kwa mechi ya kwanza ya maandalizi na kufahamu tupo kwenye hatua gani ya maandalizi, kwa hiyo natumaini tutaendelea kufanya vizuri zaidi na ilikuwa mechi yenye kipimo kizuri kwetu,” alisema Okrah raia wa Ghana.
Kuanza kufunga kwa mchezaji huyo kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya timu hiyo ya Ligi Kuu Misri kumeendeleza matumaini makubwa kwa mashabiki wa Simba juu ya uwezo wake ambapo msimu uliopita akiichezea Becham ya Ligi Kuu Ghana aliifungia mabao 14.
Simba ambayo iko Misri kujiandaa na msimu ujao wa 2022/23 imeeleza kuwa inatarajia kuumana na timu ya taifa ya Misri ya vijana chini ya miaka 20 hivi karibuni ikiwa ni miongoni mwa michezo mitatu waliyopanga kucheza wakiwa nchini humo.
Soka Okrah afurahia bao la kwanza Simba
Okrah afurahia bao la kwanza Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
