Casablanca, Morocco
Kocha wa timu ya Taifa ya Morocco, Walid Regragui amemuita katika kikosi chake beki wa PSG, Achraf Hakimi licha ya beki huyo kutuhumiwa kubaka msichana.
Morocco inajiandaa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Brazil na Peru na ingawa uteuzi wa Hakimi unaacha maswali kwa baadhi ya watu, Regragui amesema mchezaji huyo anaungwa mkono Morocco.
“Kwa upande wetu pamoja na watu wote wa Morocco tupo pamoja na Achraf,” alisema Regragui katika mkutano wake na waandishi wa habari wakati akitangaza kikosi hicho jana Jumatatu.
“Ana haki zote za kutokuwa na hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo,” alisema Regragui akitetea uamuzi wa kumuita Hakimi ambaye alikuwa katika kikosi cha Morocco kilichoweka historia kwa kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia Desemba mwaka jana.
Waendesha mashitaka nchini Ufaransa wanaendelea na uchunguzi na tayari wamewasilisha maelezo ya awali dhidi ya Hakimi akidaiwa kumbaka msichana wa miaka 24.
Hatua hiyo ya waendesha mashitaka ilikuja baada ya msichana huyo kutoa taarifa polisi akidai alibakwa nyumbani kwa Hakimi ingawa wakili wa Hakimi amesema tuhuma hizo ni sehemu ya mchezo mchafu.
Hakimi hata hivyo mbali na kuitwa timu ya Taifa ya Morocco pia alikuwamo katika kikosi cha PSG kilichoumana na Bayern Munich katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita na anaendelea kuishi nchini Ufaransa.
“Nazungumza na Achraf mara kwa mara kama ilivyo kwa wachezaji wengine wengi, yupo katika utulivu na hilo ndilo jambo muhimu, ni mtu imara uwanjani na hata nje ya uwanja, ni lazima tufikirie kuhusu soka kwanza, ana watu ambao wanasimamia mambo yake,” aliongeza Regragui.
Morocco itakuwa mwenyeji wa Brazil katika mechi itakayopigwa Tangier Machi 25 na siku tatu baadaye itaumana na Peru mjini Madrid, Hispania.