Manchester, England
Winga wa zamani wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs amesema hajawahi hata mara moja kumpiga mpenzi wake ingawa amekiri kwamba hajawahi kuwa mwaminifu kwa wapenzi wake, kwa maana nyingine amekiri kuwa na tabia za kuchepuka.
Giggs anayekabiliwa na tuhuma za kumpiga, kumdhalilisha na kuwa na tabia za kibabe dhidi ya aliyekuwa mpenzi wake, Kate Greville alikuwa akijibu swali aliloulizwa mahakamani jana kama tuhuma anazohusishwa za kutokuwa mwaminifu kwenye mapenzi na kujirusha na wanawake ovyo ni tabia za kawaida kwake.
Giggs aliulizwa na wakili wake, Chris Daw kama aliwahi kuwa na tabia ya kukosa uaminifu kwa wapenzi wake na kuwahi kuchepuka, alikiri na kufafanua kwamba amewahi kuchepuka tena si mara moja na alipoulizwa kama amewahi kupiga mwanamke, alipinga jambo hilo akisisitiza kwamba hajawahi kushindwa kujizuia hasira hadi kufikia hatua ya kupiga mwanamke.
Na hata alipoulizwa kama amewahi kumfanya Kate kama mtumwa wa kumridhisha kwa mahitaji yake, Giggs alikana jambo hilo.
Giggs pia aliielezea mahakama hiyo namna alivyokutana kwenye nyama choma na aliyekuwa mkewe Stacey ambaye wameachana wakati huo akiwa na miaka 18 na kuanza mahusiano akiwa na miaka zaidiya 20 kabla ya kuanza kuishi pamoja katika nyumba ya Giggs iliyopo Manchester. Aliiambia mahakama kwamba yeye na aliyekuwa mkewe walibahatika kupata watoto wawili na hadi sasa wameendelea kuwa marafiki wazuri.
Akimzungumzia Kate, Giggs aliiambia mahakama kuwa mapenzi yake na Kate yalishamiri baada ya wote kuelezana ukweli kwamba wametoka katika ndoa ambazo hazikuwa vizuri na alikiri kwamba hakuwahi kuwa mwaminifu kwa Kate na hakuwahi kumwambia chochote kuhusu tabia yake ya siku za nyuma ya kukosa uaminifu kwa wapenzi wake.
“Siku ya kwanza kumuona Kate nilivutiwa naye hapo hapo, nilimuona ni mwanamke aliyekuwa akivutia, nilijipa imani kwamba ni muelewa, nilijipa imani kwamba anapenda kufurahi,” alisema Giggs na kuongeza kwamba alijenga dhana kwamba Kate anahamasisha na ndipo walipoanza kujirusha, kwanza ilikuwa kwenye hoteli moja jijini London na wakawa wanaonyeshana picha wakiwa katika safari zao.
Kwa mujibu wa Giggs baada ya mapenzi kukolea ndipo kila mmoja alipoanza kuzungumzia jinsi asivyokuwa na raha kwenye ndoa yake.
Alisema kwamba tangu ajirushe na Kate kwenye hoteli moja jijini London alikuwa ametoka kuachana na mume wake kwa kipindi kisichozidi miezi sita.
Giggs alisema kwamba ingawa ndoa yake ilikuwa inapitia kipindi kigumu lakini aliendelea kuishi katika nyumba moja na familia yake akiwa na mkewe Stacey na watoto wake wawili wakati huo huo alikuwa akiendelea kujirusha na Kate.
Giggs (48) anadaiwa kumpiga mkewe Kate (36) na mdogo wake Emma (26) tukio ambalo anadaiwa kulifanya Novemba 2020, ikiwa ni miongoni mwa matukio kadhaa ya kibabe na udhalilishaji kijinsia anayohusishwa nayo dhidi ya mpenzi wake. Giggs ambaye pia alikuwa kocha wa timu ya Taifa ya Wales amelazimika kujiuzulu nafasi hiyo kwa alichodai kwamba hataki kesi hiyo iathiri kwa namna yoyote maandalizi ya timu ya Wales kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Doha, Qatar, Novemba mwaka huu.
Kimataifa Giggs akiri kuchepuka, akana kupiga mwanamke
Giggs akiri kuchepuka, akana kupiga mwanamke
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
