Barcelona, Hispania
Lewandowski hatimaye ameondoka Bayern Munich na kutua Barcelona akitimiza azma yake ya kutaka changamoto mpya baada ya kuichezea Bayern kwa miaka minane huku akiacha rekodi ya kipekee ya mabao ambayo inawafunika mastaa wengi wa soka barani Ulaya.
Kwa haraka haraka miaka minane ya Lewandowski imekuwa na rekodi kubwa ya mabao kuwazidi hata kina Lionell Messi na Cristiano Ronaldo kama utaamua kuangalia walichokifanya kwa kipindi cha miaka minane ya mafanikio yao katika soka.
Kwanza anaondoka katika Ligi Kuu Ujerumani au Bundesliga akiwa mfungaji bora wa msimu wa 2021/22 akiwa amezifumania nyavu mara 35, rekodi ambayo hapana shaka sasa mashabiki wanasubiria kumuona nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Poland akiiendelea akiwa na jezi ya Barcelona kwenye Ligi Kuu Hispania yaani La Liga.
Tuzo ya mfungaji bora kwa Lewandowski katika Bundesliga imekuwa ni kama mali yake kwani anashika rekodi ya kuibeba mara saba katika miaka yake minane, rekodi ambayo Messi na Ronaldo ambao miaka ya hivi karibuni wamekuwa gumzo duniani kote hakuna kati yao aliyeweza kuifikia.
Miaka minane iliyopita, Bayern ilimsajili Lewandowski akiwa mchezaji huru baada ya kuichezea kwa mafanikio Borussia Dortmund pia ya Ujerumani lakini sasa anaondoka akiwa amefunga jumla ya mabao 344 katika mashindano yote aliyoiwakilisha timu hiyo akishika nafasi ya pili katika historia ya timu hiyo kinara akiwa ni Gerd Muller.
Katika msimu wa 2020/21, Lewandowski hakuishia tu kuchukua tuzo ya mfungaji bora wa Bundesliga bali pia aliweka rekodi ya kufunga mabao 41 katika msimu mmoja na hivyo kuvunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Muller kwa muda mrefu, ni rekodi ambayo Messi na Ronaldo hawajawahi kuifikia.
Inatosha tu kusema kwamba Lewandowski ametua Barca akiwa shujaa wa mabao, akiifanya Bayern itawale soka la Ujerumani na kutikisa vigogo Ulaya hasa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini sasa anayaanza maisha mapya katika timu ambayo inahaha kurudisha hadhi na heshima yake Ulaya baada ya kuyumba katika miaka ya karibuni.
Barca inadaiwa kutoa Euro milioni 45 kumpata Lewandowski, pamoja na hali yao kuwa ngumu kiuchumi lakini hawakusita kumchukua mchezaji huyo na hapana shaka kwa rekodi zake ni wazi wanaamini anastahili kulipiwa ada hiyo huku wakitarajia kupata mafanikio kupitia kwake kama alivyofanya akiwa Bayern.
Kimataifa Rekodi za Lewandowski usipime
Rekodi za Lewandowski usipime
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
