Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Hemed Morocco amesema kikosi chake kimeonesha morali na kimeanza kuzoea mbinu wanazoelekezwa katika maandalizi ya mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Uganda utakaochezwa Ijumaa hii.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo wa mkondo wa kwanza utakaochezwa nchini Misri, Morocco alisema tayari wachezaji wameshawasili na kuanza mazoezi na lengo ni kuhakikisha wanapata matokeo.
“Ni mechi isiyotabirika lakini sisi tunajipanga na tayari wachezaji wamewasili na kuanza mazoezi wakiwa katika ari na morali hali ya juu, kitu ambacho kinaleta faraja kwetu,” alisema.
Morocco (pichani juu) alisema watapambana kuhakikisha wanaweka kila kitu sawa na kupata ushindi katika mechi hiyo ya kwanza itakayooonesha dira ya mwelekeo wao.
Naye nahodha msaidizi, kipa Aishi Manula alisema kwa namna wachezaji wanavyoonesha ari kwenye mazoezi anaamini watafanya vizuri katika mchezo huo kabla ya kurudi kujiandaa na mechi ya marudiano itakayopigwa Machi 28, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
“Tunashukuru tumefika salama na wachezaji wengi tayari wamewasili na kuanza mazoezi, wakionesha ari na kufanya mazoezi ya nguvu, naamini hadi siku ya mchezo tutakuwa imara na tayari kwa mapambano,” alisema Manula
Tanzania inashika nafasi ya tatu na Uganda ya mwisho kundi F, zote zikiwa na pointi moja baada ya kila mmoja kucheza michezo miwili na kuambulia kipigo kimoja na sare moja. Kinara wa kundi ni Algeria yenye pointi sita ikifuatiwa na Niger yenye pointi mbili.