Na mwandishi wetu
Bao pekee la Prince Dube limeiwezesha Yanga kutoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya TS Galaxy ya Afrika Kusini katika mechi ya kujipima nguvu iliyopigwa Jumatano ya Julai 23, 2024 kwenye Uwanja wa Kanyamazane, Afrika Kusini.
Dube, mshambuliaji wa zamani wa Azam FC alifunga bao hilo pekee dakika ya 55 na kuiwezesha Yanga kupata ushindi ikiwa ni siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 2-1 na FC Augsburg ya Ujerumani.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi katika mechi dhidi ya Galaxy alikuwa kama mwenye kujaribu wachezaji wake na kutafuta mfumo sahihi kutokana na mabadiliko aliyoyafanya hasa kuanzia kwa makipa.
Katika makipa, kocha huyo kutoka Argentina alianza kwa kumpanga Abutwalib Mshery na baadaye alimbadili na nafasi yake kuingia kipa mpya, Khomein Aboubakar ambaye naye alitolewa na kuingia kipa namba moja, Djigui Diarra.
Katika wachezaji wa ndani, Gamondi alianza na kikosi kilichokuwa na Kibwana Shomary, Dickson Job, Aziz Andambwile, Salum Aboubakar, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Farid Mussa, Denis Nkane na Shekhan Ibrahim.
Gamondi aliendelea kufanya mabadiliko ya hapa na pale kwa wachezaji wa ndani ikiwamo kumtoa Shekhan ambaye nafasi yake aliingia mshambuliaji mwingine mpya wa timu hiyo, Jean Baleke.
Kikosi hicho kiliweza kuonesha uhai kwa kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga kabla ya kupata bao hilo pekee lililoihakikishia ushindi.
Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu NBC wapo Afrika Kusini wakijinoa kwa msimu mpya wa 2024-25 na Jumapili ijayo wataumana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika mechi ya Kombe la Toyota.
Kimataifa Yanga yatamba Afrika Kusini
Yanga yatamba Afrika Kusini
Read also
