Na mwandishi wetu
Miamba ya soka nchini Simba kesho itakuwa ugenini Uwanja wa Sokoine, Mbeya kukabiliana na wenyeji wao Tanzania Prisons, huku kocha wa Wekundu hao, Juma Mgunda akieleza kuwa licha ya ugumu wa mchezo huo lakini vijana wake wako tayari kwa mapambano.
Simba itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa bao 1-0 na Prisons walipokutana kwenye ligi mara ya mwisho msimu uliopita.
Mgunda ambaye ni mechi yake ya pili kuiongoza timu hiyo baada ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nyassa Big Bullets ya Malawi kwenye mchezo wa hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mgunda, alisema mazoezi ya siku moja waliyoyafanya baada ya kurejea kutoka Malawi yamewaimarisha na kuwaondoa uchovu wa safari wachezaji wake na anaamini watapambana kupigania pointi tatu muhimu hiyo kesho.
“Mchezo utakuwa mgumu kutokana na rekodi za timu hizi mbili zinapokutana, upande wetu Simba maandalizi yetu yamekwenda vizuri na wachezaji wangu wote wapo tayari kwa mchezo huu ambao kusudio letu namba moja ni ushindi na kupata pointi tatu,” alisema Mgunda.
Kocha huyo alisema kwa muda ambao amekaa na timu hiyo tayari ameanza kuwasoma wachezaji wake na kujenga muunganiko mzuri ndani ya timu hiyo akiwataka mashabiki wa Simba watarajie mambo makubwa.
Naye Kocha Mkuu wa Prisons, Patrick Odhiambo alisema: “Tumekuwa na mwendo wa pole tangu kuanza msimu mpya mchezo uliopita, tumetoka sare ya Mbeya City lakini mchezo wa leo dhidi ys Simba ndio tunatarajia utuinue kwa kutupa pointi tatu, pia tukitaka kuendeleza rekodi yetu dhidi yao,” alisema Odhiambo.
Simba itashuka dimbani wakiwa na pointi saba mkononi baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja huku Prisons wakiwa na pointi nne baada ya kushinda mchezo mmoja, sare moja na kupoteza mechi moja, ikishikilia nafasi ya nane.
Soka Simba ipo Mbeya kulipa kisasi
Simba ipo Mbeya kulipa kisasi
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
