Madrid, Hispania
Rais wa La Liga, Javier Tebas amesema anamkaribisha mara ya pili kocha Jose Mourinho katika soka la Hispania huku kukiwa na habari kwamba kocha huyo anaweza kurudi mara ya pili katika klabu ya Real Madrid.
Rais wa Real Madrid, Florentino Pérez inadaiwa anamfikiria kocha huyo ambaye anainoa Benfica ili achukue nafasi ya kocha wa sasa Álvaro Arbeloa mara baada ya msimu huu kumalizika.
Tebas amenukuliwa akisema kwamba kama Real Madrid na viongozi wao wataamua hivyo hilo litakuwa jambo zuri kwa Real Madrid kwani Mourinho wakati wote ni mtu wa kujiweka juu na hilo ni jambo zuri kwa La Liga.
Katika misimu mitano ambayo Mourinho amekuwa kocha Real Madrid, ameiwezesha timu hiyo kubeba mataji ya La Liga, Spanish Supercup na Copa del Rey kabla ya kuachana nayo mwaka 2013 kwa makubaliano ya kiungwana na Perez.
Mourinho, 63, ana mkataba na Benfica unaofikia ukomo Juni 2027 lakini katika mkataba huo kuna kipengele ambacho kinairuhusu klabu au kocha huyo kuvunja mkataba mwishoni mwa msimu huu.
Januari mwaka huu baada ya kutimuliwa kwa Xabi Alonso, Madrid ilimpa majukumu ya ukocha Arbeloa, mchezaji wa zamani wa timu hiyo aliyewahi kufundishwa na Mourinho.
Kwa namna msimu huu wa 2025-26 unavyoendelea Madrid inasubiri kumaliza msimu wa pili bila taji hivyo moja ya mikakati yao msimu ujao ni kuwa na kocha wa hadhi na Mourinho ni kati ya makocha walio katika hesabu zao.
Kimataifa Bosi La Liga amtaka Mourinho
Bosi La Liga amtaka Mourinho
Read also
