Perth, Australia
Kipa wa Man United, David De Gea ameeleza kuchoshwa kwake na tuzo anazopata za mchezaji bora wa mwaka kila wakati timu hiyo inapokuwa na msimu mbaya.
De Gea ameshinda mara nne tuzo ya Sir Matt Busby ikiwamo mara tatu mfululizo katika kipindi cha mwaka 2014 na 2016 na sasa anakiri kwamba atakuwa mwenye furaha kama hatashinda tuzo hiyo tena.
Katika kulielezea hilo, De Gea aliunga mkono kauli iliyowahi kutolewa na kocha Jose Mourinho wakati akiwa kocha wa Man United pale aliposema kwamba inapotokea kipa anashinda tuzo hiyo ni dalili ya kwamba timu haijacheza vizuri.
“Hakika nakubaliana kabisa na hilo, kweli kwangu inaweza kuwa kitu kizuri, napenda kushinda makombe lakini nakubaliana na kile alichosema Mourinho, inatakiwa tuzo iwe kwa mshambuliaji, mchezaji wa kiungo, hivyo ndivyo inavyokuwa lakini kwa hakika msimu huu itakuwa kwa mchezaji mwingine, hiyo ni hakika.” alisema De Gea.
De Gea anaingia katika msimu wake wa 12 akiwa Man United na katika kipindi chote hicho ameshinda taji moja tu la Ligi Kuu England, moja la FA, moja la Ligi na moja la Europa Ligi akiwa amecheza mechi 486 za michuano mbalimbali hadi sasa.
Mwaka 2015 kipa huyo alihusishwa na mipango ya kujiunga na klabu ya Real Madrid, mipango ambayo ilivuma kabla ya kukwama lakini De Gea mwenyewe anasisitiza kwamba hana anachojuta kwa kukosa nafasi ya kujiunga na Real Madrid ambayo tangu wakati huo hadi sasa imeshinda mataji matatu ya La Liga, na manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Kushinda au kutoshinda taji si hoja, kitendo cha kuwa tu katika klabu hii kuna maana kubwa kuliko kushinda mataji lakini ukweli ni kwamba tunataka kushinda mataji, wakati wote tunataka kushinda lakini kuiwakilisha klabu hii ni jambo kubwa kuliko taji lolote.” alisema De Gea akionekana kujifariji.
