Manchester, England
Mmoja wa wamiliki wa klabu ya Manchester United, Sir Jim Ratcliffe amesema anaweza kuachana na klabu hiyo kama atakuwa mwenye kudhalilishwa na mashabiki kama ilivyokuwa kwa familia ya Glazer.
Ratcliffe, bilionea maarufu Uingereza, mwaka jana alitoa Pauni 1.3 bilioni na kununua asilimia 28.93 ya hisa za klabu hiyo na kumfanya awe na jukumu la kusimamia mambo ya soka.
Katika mazugumzo yake hivi karibuni, Ratcliffe, bilionea ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 72 alinukuliwa akisema kwamba hatojali hata kama hatokuwa na umaarufu.
Mapema mwezi uliopita kulikuwa na taarifa kwamba klabu hiyo ina mpango wa kupunguza gharama ambapo wafanyakazi takriban 200 wataachishwa kazi, hiyo ni mbali na wengine 250 walioachishwa kazi mwaka jana.
Sambamba na hilo pia kumekuwa na ongezeko la bei ya tiketi katikati ya msimu, jambo ambalo linawaathiri watoto wa umri chini ya miaka 16 pamoja na wazee wastaafu.
Jumatatu iliyopita, Ratcliffe alinukuliwa akisema kwamba kuna wachezaji wa klabu hiyo ambao si wazuri na wanalipwa fedha nyingi na kwamba klabu ipo katika muelekeo mbaya.
Siku moja baadaye, Ratcliffe alitangaza mpango wa klabu hiyo kujenga uwanja mpya ambao utachukua watu 100,000 ambapo Pauni 2 bilioni zinatarajiwa kutumika katika mpango huo.
“Namaanisha naweza kuachana na haya mambo, sijali kutokuwa maarufu kwa sababu hakuna anayependa kuiona Manchester United inakuwa chini ilipo na hakuna anayependa maamuzi tunayoyachukua kwa sasa,” alisema Ratcliffe.
Bilionea huyo alisema anaweza kuchoshwa kwa sababu na yeye hana tofauti yoyote na mtu wa kawaida kwa kuwa kinachoendelea si kizuri hasa kwa marafiki na familia.
“Kwa hiyo kama itafikia kiwango ambacho familia ya Glazer ilikutana nacho katika kudhalilishwa nitalazimika kusema jamani imetosha, ngoja mwingine aje,” alisema Ratcliffe.
Mara baada ya Ratcliffe kununua hisa Man United, mashabiki wengi walimpokea kwa furaha bilionea huyo ambaye ni shabiki wa klabu hiyo tangu utotoni wakimkaribisha kwa imani kwamba atasaidia kuweka mambo sawa.
