Na mwandishi wetu
Siku moja baada ya kuachana na kocha Kally Ongalla, uongozi wa Azam FC umeeleza kuwa upo kwenye mikakati kabambe kuisuka timu hiyo ikiwemo kushusha wachezaji hatari kuelekea msimu ujao.
Kally aliyekuwa kocha wa washambuliaji kabla ya kuwa kocha msaidizi aliachwa ikiwa ni msimu mmoja baada ya kuwa na timu hiyo ingawa aliwahi kuwa kocha wa timu hiyo miaka ya nyuma.
Ofisa Habari wa Azam, Hasheem Ibwe amesema kwa sasa wanaweka sawa benchi lao la ufundi na kikosi cha timu hiyo kwa baadhi yao kuagana nao ili kutengeneza timu tishio kwenye michuano ya nyumbani na ya klabu Afrika msimu ujao.
“Kwa sasa tumeendelea kuwashukuru baadhi ya tuliokuwa nao, tunaweka mazingira sawa kwa ajili ya msimu ujao, tumemalizana nao kwa wachezaji kuangalia changamoto mpya na klabu pia kutafuta wachezaji wakali watakaotupeleka nchi ya ahadi,” alisema Ibwe.
“Tumelenga kuwa na wachezaji mahiri mno kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao kwenye michuano ya kimataifa na kujiimarisha kwenye michuano ya ndani, tuna mpango wa kuleta wachezaji ambao wengine wanadhani wanaweza kucheza Afrika, mchakato ni mkubwa juu ya hilo,” alisema Ibwe.
Azam ambayo imemaliza nafasi ya tatu Ligi Kuu NBC na kufika fainali ya Kombe la FA (ASFC) msimu huu, pia imeachana na kocha wa makipa, Dani Cadena.
Kwa upande wa wachezaji walioachwa ni pamoja na Bruce Kangwa, Rodgers Kola, Kenneth Muguna, Ismail Aziz na Cleophas Mkandala.