Roma, Italia
Kocha wa Roma, Jose Mourinho ameamua kujiondoa katika bodi ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) ikiwa ni siku chache baada ya kufungiwa mechi nne zinazoandaliwa na shirikisho hilo.
Mourinho alifungiwa akidaiwa kumbughudhi ikiwamo kumkoromea mwamuzi Anthony Taylor katika mechi ya fainali ya Europa Ligi dhidi ya Sevilla, mechi ambayo Roma ililala kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1-1.
Mourinho alionekana kutoridhishwa na maamuzi ya Taylor na hata baada ya mechi alimfuata mwamuzi huyo hadi kwenye eneo la kupaki magari huku ikiaminika kuwa alimshambulia kwa maneno makali.
Katika kujitoa katika bodi hiyo, Mourinho aliandika barua iliyosomeka, “Nawashukuru kwa kunipa mwaliko na kuwa mjumbe ya bodi ya Uefa, nasikitika kuwaarifu kwamba kuanzia sasa natangaza kujitoa ushiriki wangu katika kundi hilo.”
“Mazingira ambayo niliyaamini kwa nguvu zote wakati najiunga hayasimamiwi tena na najiona ni mwenye kuwajibika kuchukua uamuzi wa kujitoa, nawaomba pia muufikishe ujumbe wangu kwa Rais wa Uefa, Aleksander Ceferin, ” alisema Mourinho katika barua yake.
Mbali na adhabu aliyopewa Mourinho, Uefa pia imeipiga marufuku klabu ya Roma kuuza tiketi kwenye mechi ijayo ya ugenini ya Uefa, klabu hiyo pia imetozwa faini ya Dola 55,000 kwa makosa ya kurusha vitu uwanjani na kulipua fataki.
Siku moja baada ya mechi hiyo, Taylor na familia yake walibughudhiwa na kuzomewa na mashabiki wanaoaminika kuwa ni wa Roma kwenye Uwanja wa Ndege wa Budapest.