Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Simba leo Jumamosi umemtambulisha rasmi kiungo mkabaji mpya wa timu hiyo, Babacar Sarr raia wa Senegal aliyesaini mkataba wa miaka miwili.
Usajili wa Sarr umekuwa gumzo siku za karibuni huku baadhi ya picha zake zikimuonesha akikabiliana na winga wa zamani wa Man United, Cristiano Ronaldo ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia.
Kiungo huyo ametua Simba akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na US Monastir ya Tunisia aliyoitumikia msimu uliopita katika michuano ya Ligi Kuu Tunisia na Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu hiyo ilitolewa hatua ya robo fainali.
Akizungumzia usajili huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema usajili huo ni pendekezo la kocha wao mkuu, Abdelhak Benchikha kutokana na kufahamu vizuri ubora wa mchezaji huyo.
“Usajili wa Sarr ni pendekezo la kocha Benchikha, ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, mashindano aliyocheza na aina ya washambuliaji aliokabana nao inaeleza kwamba huu ni usajili ambao utakuwa na tija kwetu kuelekea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na harakati za kurudisha mataji yetu yote ya ndani,” alisema Ally.
Huyo anakuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kusajiliwa na Simba kwenye dirisha dogo la msimu huu baada ya wiki iliyopita kumtambulisha mzawa Salehe Karabaka kutoka JKU ya Zanzibar kwa mkataba wa miaka mitatu.