Doha, Qatar
Nahodha wa timu ya Ufaransa, Hugo Lloris amesema kwamba ‘hamasa na shauku’ ya kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Argentina itawasaidia wachezaji wenzake kuepukana na hofu ya uwapo wa virusi katika kambi ya timu hiyo.
Wachezaji wa timu ya Ufaransa, Raphael Varane, Ibrahima Konate na Kingsley Coman wamelazimika kufanya mazoezi wakiwa mbali na wachezaji wenzao baada ya kuonyesha dalili za kuwa wagonjwa huku wakihusishwa na virusi vinavyodaiwa kuingia katika kambi ya timu hiyo.
Katika tukio linalohusishwa na virusi hivyo wachezaji, Coman, Dayot Upamecano na Adrien Rabiot walijikuta wakiikosa mechi ya nusu fainali Jumatano iliyopita dhidi ya Morocco huku tatizo likihusishwa na virusi hivyo ingawa kocha Didier Deschamps ana matumaini ya kuwa na wachezaji hao watatu katika mechi ya fainali leo baada ya jana Jumamosi jioni kufanya mazoezi.
Ufaransa leo inaumana na Argentina kwenye Uwanja wa Lusail huku timu hiyo ikiwa imepania kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza duniani kulitetea taji la dunia baada ya Brazil kufanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 1962.
“Kuhusu virusi huwezi katu kujiandaa kwa jambo hilo lakini tunajaribu kuwa tayari kwa ajili ya hii mechi kadri tunavyoweza, hili la virusi ni jambo ambalo hatukuwa tumejiandaa nalo lakini tunaendelea kuwa makini na tayari na hakika tumehamasika kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Dunia,” alisema Lloris, kipa namba moja wa timu hiyo.
“Nafikiri huko nyuma tumethibitisha kwamba timu za Ufaransa ambazo zimepata mafanikio wakati wote mafanikio hayo msingi wake ni ari iliyopo kwenye timu. Kwa hiyo tunajaribu kujiweka tayari kwa hilo, kuna mtazamo mzuri katika kambi yetu tangu kuanza kwa michuano hii na hatuoni ni kwa nini hali isiendelee kuwa hivyo hivyo kesho (leo),” alisema.
Kwa upande wake, Deschamps katika mkutano wake wa jana hakutaka kuzungumzia kuhusu wachezaji wake na kama kuna majeruhi au wanaosumbuliwa na virusi kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na vyanzo mbalimbali vya habari badala yake alisema kuna tukio dogo la dalili za maradhi ya mafua ambalo wamekuwa wakijitahidi kulizuia lisiwakute wengi.
Habari za ndani zinadai kwamba Varane alionyesha dalili za kuwa na virusi pamoja na beki mwenzake, Ibrahima Konate ambao wote wameendelea kubaki kwenye vyumba vyao wakidaiwa kusumbuliwa na virusi hivyo.
Mchezaji mwingine wa Ufaransa, Ousmane Dembele akizungumza na waandishi wa habari juzi alisema kwamba wachezaji wa timu hiyo hawana wasiwasi wowote kuhusu virusi vinavyodaiwa kuwakumba baadhi ya wachezaji katika timu hiyo.
Wakati habari ya virusi ikitawala timu ya Ufaransa, habari kubwa nyingine duniani kwa sasa ni kuhusu nahodha wa Argentina, Lionel Messi mwenye umri wa miaka 35 ambaye huenda hizi zikawa fainali zake za mwisho za Kombe la Dunia huku akipewa matumaini makubwa ya kubeba kombe dhidi ya mabingwa watetezi, Ufaransa.
Kimataifa Lloris aipotezea hadithi ya virusi
Lloris aipotezea hadithi ya virusi
Read also