Yaounde, Cameroon
Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon na Man United, Eric Djemba Djemba (pichani) amesema kipa wa Man United na timu ya taifa ya Cameroon, Andre Onana lazima afikirie soka lake pale anapoamua kukosa baadhi ya mechi za Ligi Kuu England (EPL).
Onana atakosekana katika EPL kwa takriban mwezi mmoja kama atajiunga na timu ya taifa ya Cameroon kwenye fainali za Afcon zitakazoanza Januari mwakani nchini Ivory Coast.
Septemba mwaka huu, Onana alitangaza kufuta uamuzi wake wa awali wa kustaafu kuichezea timu ya Cameroon, kwa sasa anapitia kipindi kigumu Man United baada ya kuwa katika msimu mgumu ambapo timu hiyo imetolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na katika EPL mambo si mazuri.
“Moja ya tatizo kwake ni kwamba hata akicheza vizuri kwa kipindi hiki bado atakuwa nje kwa mwezi mmoja kwa ajili ya Afcon,” alisema Djemba Djemba na kuongeza kuwa Onana pia anaweza akajiharibia nafasi yake ya kuwa kipa namba moja wa Cameroon kama atabaki Man United kipindi cha Afcon.
“Anajua kwamba kama akienda kwenye Afcon anaweza akapoteza nafasi yake Manchester United, anatakiwa kuamua kipi bora kwake, anachotakiwa ni kufanya kile kilicho bora kwa soka lake,” alisema Djemba Djemba.
Fainali za Afcon zitaanza rasmi kutimua vumbi Januari 13 na kufikia tamati Februari 11 ambapo Onana akienda huko atakosa zaidi ya mechi nne za EPL za Man United kutegemea na nafasi ya Cameroon kwenye Afcon kama itafika mbali au itaishia hatua ya makundi.
Onana (pichani chini) alisajiliwa Man United Julai mwaka huu kwa ada ya Pauni 47 milioni akitokea Inter Milan lakini amejikuta akilaumiwa kwa makosa yaliyoigharimu timu hasa kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray na Bayern Munich.
“Kila mtu anaijua Manchester United, ni moja ya timu kubwa duniani, unapojiunga Manchester United hawakupi muda” alisema Djemba Djemba aliyewahi kuichezea timu hiyo baada ya kujiunga nayo mwaka 2003, alicheza mechi 39 chini ya kocha mkongwe, Sir Alex Ferguson.
Djemba Djemba alisema tatizo la Onana katika timu hiyo linachangiwa na uchezaji wake wa kutoa pasi karibu na eneo lake jambo ambalo halipendelewi Man United.
“Ni kipa mmoja au wawili wa Manchester City wanaocheza kwa staili hiyo ya kutoa pasi, wana kocha Pep Guardiola, anapenda kipa wa aina hiyo ambaye anacheza zaidi kwa miguu,” alisema Djemba Djemba.
“Kwa Manchester United ukiwa kipa mzuri kwa kutumia mikono yako watakusajili, hawatajali kama huna tabia ya kutumia miguu kutoa pasi, Onana amejikuta akilaumiwa kwa sababu Manchester United ni timu kubwa,” alisema Djemba Djemba.