Brussel, Ubelgiji
Kiungo wa timu ya Taifa ya Ufaransa, N’Golo Kante (pichani) amenunua klabu ya soka ya daraja la tatu nchini Ubelgiji ya Royal Virton na sasa anakuwa mwenyekiti rasmi wa klabu hiyo.
Kante mwenye umri wa miaka 32 ambaye hivi karibuni ameamua kuihama Chelsea na kujiunga na klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia atakabidhiwa rasmi uenyekiti wa klabu hiyo Julai Mosi kutoka kwa Flavio Becca, siku ambayo pia atajiunga na Al-Ittihad.
“Flavio ni mwenye furaha kwa kuwa tayari kukabidhi funguo za klabu kwa N’Golo Kante,” ilieleza taarifa ya klabu ya Royal Virton.
“Ni mchezaji wa kiwango cha juu, si tu kutokana na uwezo wake lakini pia anafahamika kwa namna ya kipekee kwa kuwa na sifa za ubinadamu,” ilieleza zaidi taarifa ya klabu hiyo.
Royal Virton kwa sasa inakamilisha taratibu za kuipata kwa mara nyingine leseni yake na itacheza katika Ligi ya Taifa ya Ubelgiji katika msimu wa 2023-24.
Ligi hiyo ya Taifa, ni miongoni mwa ligi za soka za nchini Ubelgiji ingawa juu yake kuna ligi nyingine mbili kubwa.
Haijaelezwa hata hivyo Kante ameinunua klabu hiyo kwa kiasi gani cha fedha zaidi ya taarifa kubainisha kwamba Royal Virton haina madeni yoyote.
Kimataifa N’Golo Kante anunua klabu ya soka
N’Golo Kante anunua klabu ya soka
Related posts
Read also
