Brussels, Ubelgiji
Kipa wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Thibaut Courtois (pichani) sasa ni rasmi kuwa hatoweza kuiwakilisha timu hiyo kwenye fainali za Euro 2024 kutokana na matatizo ya goti yanayomkabili.
Habari hizo zimekuja huku kukiwa na habari nyingine zinazodai kwamba kipa huyo huenda akawa tayari kuichezea klabu yake ya Real Madrid katika mechi chache zilizobaki za msimu huu.
Courtois, 31, amekosekana uwanjani msimu huu wote na mwezi Machi mwaka huu, mchezaji huyo alihitaji kufanyiwa operesheni nyingine baada ya kuonekana kulikuwa na tatizo lililofanya asiweze kuwa fiti.
Akimzungumzia kipa huyo na habari za uwezekano wa kurudi kwenye kikosi cha Real Madrid kwa msimu huu, kocha wa Ubelgiji, Domenico Tedesco alimfuta moja kwa moja katika hesabu zake kwa ajili ya fainali za Euro 2024.
Desemba mwaka jana, Courtois ambaye ameichezea Ubelgiji mara 102 alisema kwamba anadhani hatokuwa amepona kwa asilimia 100 kwa ajili ya kuiwakilisha Ubelgiji kwenye fainali za Euro 2024 zitakazofanyika nchini Ujerumani kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu.
Kwa upande wake, Tedesco alisema kwamba suala la kipa huyo limekwisha, “kuhusu habari hiyo kila kitu kimeshasemwa, sitaki kurudiarudia, tunawaangalia wachezaji ambao wapo katika ubora.”
Naye kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amenukuliwa akisema kwamba ana matumaini ya kipa huyo kuwamo katika kikosi cha Real Madrid kitakachoumana na Cadiz Jumamosi ijayo katika mechi ya La Liga.
Kikapu Thibaut Courtois kukosa Euro 2024
Thibaut Courtois kukosa Euro 2024
Read also