Na mwandishi wetu
Yanga imemaliza mechi zake za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika Ijumaa hii kwa kukutana na kipigo cha bao 1-0 mbele ya Al Ahly ya Misri ingawa timu hizo zote zimefuzu hatua ya robo fainali ya ligi hiyo.
Kwa matokeo ya mechi hiyo ambayo Yanga ilikuwa ugenini, Ahly ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo wamemaliza mechi za makundi wakiwa kinara katika Kundi B na pointi zao 12 na Yanga imeshika nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi nane.
Bao lililoizamisha Yanga lilipatikana dakika moja baada ya kuanza kipindi cha pili mfungaji akiwa ni Hussein Shehata, bao ambalo kwa kiasi kikubwa lilichangiwa na makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga.
Yanga licha ya kufungwa bao hilo pekee, ilionesha kandanda safi kuanzia mwanzo hadi mwisho huku kipa wake Djigui Diarra akionesha umahiri kwa kuokoa michomo kadhaa iliyoelekezwa langoni mwake hasa katika kipindi cha pili.
Katika mechi hiyo Yanga ilipata pigo baada ya kiungo wake, Khalid Aucho kuumia na nafasi yake kuingia Aboubakar Salum ‘Sure Boy’ ingawa haikuweza kufahamika mara moja ukubwa wa majeraha aliyopata mchezaji huyo.
Mechi nyingine ya kundi hilo ilizikutanisha CR Belouizdad ya Algeria iliyokuwa ikiumana na Medeama ya Ghana, mechi ambayo iliisha kwa Belouizdad kutoka na ushindi wa mabao 3-0.
Belouizdad ambayo kabla ya mechi hiyo ilikutana na kipigo cha mabao 4-0 mbele ya Yanga, imemaliza mechi zake za makundi ikishika nafasi ya tatu wakati Medeama ikiburuza mkia.
Kimataifa Al Ahly yaitungua Yanga 1-0
Al Ahly yaitungua Yanga 1-0
Read also