Bellinzona, Uswisi
Mabosi wawili wa zamani wa soka, Sepp Blatter wa Fifa na Michel Platini wa Uefa, leo wamepanda katika Mahakama ya makosa ya Jinai mjini Belinzona, Uswisi
Vigogo hao maarufu kwenye soka duniani wanakabiliwa na makosa kadhaa ya rushwa ikiwamo kuhusika katika malipo haramu ya Dola milioni 2.8 mwaka 2011, tuhuma ambazo wote wawili wamezikana kwa nguvu zote.
Majaji watatu wanaendesha kesi hiyo inayotarajia kusikilizwa hadi Juni 22 na hatima ya washitakiwa huenda ikajulikana Julai 8 na iwapo watakutwa na hatia watakumbana na kifungo cha jela kuanzia miaka mitano na zaidi.
Katika tuhuma hizo, mabosi hao ambao enzi zao walikuwa majina makubwa katika soka duniani, wanadaiwa kulipwa fedha hizo kati ya mwaka 1998 na 2002 ikiwa ni kwa ajili ya kazi ya ushauri.
Akizungumza mahakamani hapo kabla ya kuanza kwa kesi hiyo, Blatter alisema kwamba anajiamini, “jua linawaka na niko katika hali nzuri.” “Najua sijafanya chochote dhidi ya sheria, maisha yangu yalikuwa ni soka, kwa miaka 45 ndani ya Fifa, maisha yangu ni soka.”
Platini, ambaye pia ni mwanasoka nyota wa zamani wa Ufaransa naye alionekana mwenye kujiamini mahakamani hapo na kuwatania waandishi wa habari pale aliposema kwamba atachukua kozi ya Kijerumani ili aweze kufuatilia vizuri kesi hiyo.
“Ninaamini haki itatendeka na hivyo ndivyo itakavyokuwa kwangu baada ya miaka mingi ya tuhuma za hovyo na kuchafuliwa, tutaithibitishia mahakama kwamba nilifanya kazi kwa uadilifu.” alisema kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa.
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa Uswisi inawatuhumu Blatter na Platini kwa ufisadi, ulaghai na kughushi kwa nia ovu. Blatter na Platini wamefungiwa kujihusisha na soka kwa miaka sita tangu mwaka 2016.
Wakati Blatter mwenye miaka 85 sasa amekuwa ndani ya Fifa kwa miaka mingi akiwahi kuwa katibu mkuu na baadaye rais, Platini (66) mbali na kuwa kiongozi wa Uefa lakini amecheza soka kwa mafanikio na alikuwa nahodha wa timu ya Taifa ya Ufaransa iliyobeba taji la Ulaya mwaka 1984.
