Buenos Aires, Argentina
Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi atazikosa mechi za kirafiki za timu hiyo dhidi ya El Salvador na Costa Rica kutokana na matatizo ya misuli yanayomkabili.
Messi ambaye kwa sasa anaichezea Inter Miami FC ya Marekani wiki iliyopita alilazimika kuwekwa benchi muda mfupi baada ya kuanza kipindi cha pili katika mechi ya taji la Concacaf Championship dhidi ya Nashvile ambayo Miami ilitoka na ushindi wa 3-1.
Mchezaji huyo pia Jumamosi iliyopita alikaa benchi tangu mwanzo katika mechi ya ligi dhidi ya D.C United na kocha wake, Gerardo “Tata” Martino kuahidi kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kujua ukubwa wa majeraha yanayomsumbua mchezaji huyo.
Siku chache zilizopita jina la Messi lilitajwa katika kikosi cha Argentina kwa ajili ya mechi hizo zitakazopigwa mjini Los Angeles, Marekani lakini jana Jumatatu Chama cha Soka Argentina (AFA) kilitangaza kumuondoa mchezaji huyo aliyeiwezesha Argentina kubeba Kombe la Dunia mwaka 2022.
Taarifa ya AFA pia ilieleza kuwa Messi atakuwa karibu na timu ya taifa baadaye wiki hii ili kupata tiba na madaktari wa timu hiyo lengo likiwa ni kumfuatilia kwa karibu.
Argentina ambayo pia itawakosa mshambuliaji Paulo Dybala na kiungo Exequeil Palacio kutokana na kuwa majeruhi, imeandaa mechi hizo kujinoa kwa ajili ya michuano ya Copa America ambayo itafanyika Juni na Julai nchini Marekani.
Kimataifa Messi aondolewa timu ya taifa
Messi aondolewa timu ya taifa
Read also