London, England
Leo Jumatatu, England inaumana na Ujerumani katika mechi ya Uefa Nations Ligi, kwa kocha wa England, Gareth Southagate, mbali na mechi hiyo ameanza kufikiria hatma ya kibarua chake.
England haina matokeo mazuri katika michuano hiyo na Southgate analifahamu hilo lakini kwa sasa ameanza kuingiwa na hofu kuhusu hatma ya kibarua chake baada ya fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Novemba mwaka huu.
Southgate amesema anajua kwamba mkataba wake wa kuinoa England unafikia ukomo mwaka 2024 lakini anaamini matokeo mabaya ya kwenye fainali za Kombe la Dunia yanatosha kabisa kuwa sababu ya kibarua hicho kufikia ukomo kabla ya 2024.
Baada ya kufungwa bao 1-0 na Italia, England ilijiweka pabaya kwenye Uefa Nations Ligi Ijumaa iliyopita, mechi ya leo na Ujerumani ni mtihani mwingine mgumu kwa kocha huyo ambaye hadi sasa ana rekodi isiyovutia ya kucheza mechi tano bila kushinda hata moja jambo ambalo limetokea kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014.
“Mimi si mpumbavu, najua mwisho wa siku hatma yangu itajadiliwa kwa kile ambacho kitatokea kwenye fainali za Kombe la Dunia,” alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 52.
“Mikataba katika soka haina maana yoyote kwa sababu makocha wanakuwa na mikataba ya miaka mitatu, minne, mitano na kama matokeo si mazuri hapo unakubali kwamba huo ni wakati wako wa kuondoka, sasa kwanini kwangu iwe tofauti, sijabweteka kiasi cha kufikiria kwamba kuwa na mkataba kutanilinda kwa namna yoyote na matokeo mabaya,” aliongeza.
Southgate aliiongoza vyema England hadi kufikia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na kuifikisha katika fainali za Euro 2020 ambazo hata hivyo zilifanyika mwaka 2021 lakini kwa sasa mambo yake yanaonekana kuwa magumu.
Kocha huyo inaaminika kwamba amekuwa akiungwa mkono na mabosi wake wa FA lakini mara kadhaa amejikuta akizomewa na mashabiki kutokana na matokeo mabaya, mfano Ijumaa alizomewa timu hiyo ilipofungwa na Italia na pia alizomewa siku England ilipofungwa mabao 4-0 na Hungary.
Mechi za Uefa Nations Ligi leo Jumatatu
England v Ujerumani
Gibraltar v Georgia
North Macedonia v Bulgaria
San Marino v Estonia
Hungary v Italia
Montenegro v Finland
Romania v Bos-Herze
Kimataifa Southgate awazia kibarua chake England
Southgate awazia kibarua chake England
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
