Manchster, England
Kiungo wa Man City, Kevin De Bruyne ameachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji kwa kinachodaiwa kuwa ni kusumbuliwa na matatizo ya misuli.
De Bruyne alijikuta akiwekwa kando kwa miezi mitatu mwanzoni mwa msimu huu kutokana na mataizo ya misuli na alirudi kuiwakilisha Man City kwa mara ya kwanza Januari mwaka huu.
Mchezaji huyo sasa atazikosa mechi za timu ya taifa ya Ubelgiji dhidi ya Jamhuri ya Ireland pamoja na England zitakazopigwa wiki hii.
“Sina hakika kama ni matatizo ya misuli, ni matatizo mengine ambayo yamekuwa yakimpa tabu katika mechi kadhaa za hivi karibuni,” alisema kocha wa Ubelgiji, Domenico Tedesco katika mkutano wake na waandishi wa habari jana Alhamisi.
“Jana nilizungumza na daktari pamoja na Kevin na tukaamua hali hatarishi ni kubwa, ni jukumu letu kwa mchezaji lakini pia kwa klabu yake,” alisema Tedesco.
Kocha huyo alisema kwamba ni bora kumpa nafasi ya kupona vizuri akiwa Man City ili baadaye kuwa naye akiwa fiti kwenye fainali za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024 zitakazoanza Juni mwaka huu nchini Ujerumani.
Tedesco ambaye ameongezewa mkataba hadi Julai 2026, alikabidhiwa jukumu la kuinoa timu ya Ubelgiji baada ya fainali za Kombe la Dunia 2022 akichukua nafasi ya Roberto Martinez na tangu apewe jukumu hilo, Ubelgiji haijapoteza hata mechi moja kati ya 10 zilizopita.
Kocha huyo ambaye ameiwezesha Ubelgiji kufuzu Euro 2024 kwa kishindo hata hivyo amekuwa haivi chungu kimoja na kipa tegemeo wa timu hiyo, Thibaut Courtois ambaye hayumo katika kikosi chake.
Kikosi cha Ubelgiji kilichotangazwa na Tedesco ni kama ifuatavyo…
Makipa: Arnaud Bodart, Matz Sels, Koen Casteels, na Thomas Kaminski.
Mabeki: Koni De Winter, Timothy Castagne, Zeno Debast, Wout Faes, Jan Vertonghen, Thomas Meunier na Arthur Theate.
Viungo: Arthur Vermeeren, Olivier Deman, Jérémy Doku, Dodi Lukébakio, Orel Mangala, Amadou Onana, Youri Tielemans na Aster Vranckx
Washambuliaji: Johan Bakayoko, Leandro Trossard, Michy Batshuayi, Charles De Ketelaere, Romelu Lukaku na Loïs Openda.